Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msajili akana kuutambua uchaguzi wa TLP

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Muktasari:

  • Wakati ADC ikipata viongozi wapya, TLP imeitisha mkutano wa kumchagua mrithi wa Mrema, lakini Ofisi ya Msajili imekana kuutambua.

Dar es Salaam. Wakati Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kikipata viongozi wapya, Chama cha Labour Party (TLP) kimefanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho, huku Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ikisema haiutambua uchaguzi huo.

Jana Jumamosi, Juni 29, 2024, TLP kiliitisha mkutano mkuu, ili kujaza nafasi ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, marehemu Augustine Mrema, aliyefariki dunia Agost1 21, 2022, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam.

Mrema alikuwa mwenyekiti wa chama hicho tangu alipojiunga nacho mwaka 1999 akitokea NCCR Mageuzi.

Baada ya kifo chake, uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo ulipangwa kufanyika Februari 28, 2023 lakini uliahirishwa na kupangwa kufanyika Machi 6, mwaka huo ili kuziba nafasi hiyo, lakini pia uliahirishwa kwa kile kilichodaiwa ni changamoto ya kibajeti.

Awali, Ofisi ya Msajili iliutaka uongozi wa TLP kujibu malalamiko yaliowasilishwa na wagombea wa nafasi hiyo ya kutofanyika uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo.

Hata hivyo, Machi 6, 2023 waliokuwa wagombea wa nafasi hiyo waliwasilisha malalamiko katika ofisi ya msajili kuhusu kuvunjwa kwa mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi huo.

Machi 9, 2024, Ofisi ya Msajili ilisema imepokea barua kutoka kwa wagombea wa nafasi hiyo, wakilalamika mkutano mkuu wa chama uliokuwa umepangwa kufanyika siku hiyo uliahirishwa bila kufuata katiba na kanuni za chama chao.

Lakini jana chama hicho kiliitisha mkutano mkuu wa uchaguzi uliohusisha wagombea watano na Mwenyekiti wa Vijana Taifa, Ivan Maganza aliibuka mshindi baada ya kupata kura 35 kati ya 55 zilizopigwa na kuwashinda wagombea wengine wanne.

Wagombea hao ni Richard Lyimo aliyepata kura 0, Abun Changawa kura 0, Stanley Ndamagoba kura 10 na Kinangaro Mwanga kura 10.


Alichosema msajili

Alipotafutwa Naibu Msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza kuzungumzia hilo, amesema ofisi yake haiutambui mkutano huo kwa sababu hawana taarifa yoyote.

Amesema kwa kawaida mkutano mkuu hasa wa kujaza nafasi ya mwenyekiti, ofisi ya msajili inapaswa kufahamishwa kwa maandishi siku na tarehe ya kufanyika kwa mkutano husika.

“Chama kilichoitisha mkutano ni TLP hii ninayoifahamu mimi au nyingine, uchaguzi kama huo ni lazima ofisi yangu iwe na taarifa, jana tulikuwa tunasimamia uchaguzi wa ADC, sasa huo uchaguzi umefanyikia wapi?”amehoji Nyahoza.

Amesema mara zote kama chama hicho kinafanya uchaguzi, huwa wanapokea barua kutoka kwa katibu mkuu wa TLP ambaye ofisi inamtambua, Richard Lyimo.


Halmashauri Kuu yamtimua katibu mkuu

Wakati hayo yakijiri Ofisi ya Msajili, huko TLP baada ya kumalizika kwa uchaguzi, Halmashauri Kuu ilikutana kwa dharura na kuazimia kumuondoa Katibu Mkuu, Richard Lyimo kwenye nafasi yake na makamu wake (Bara) naye akisimamishwa na kupewa siku tano za kujieleza.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, Lyimo na makamu wake wanatuhumiwa kufanya vikao vya siri kwa ajili ya kukikwamisha chama hicho hasa kwenye uchaguzi.

 “Mbali na wajumbe hao kusimamishwa, halmashauri ilivunja bodi ya wadhamini kwa tuhuma za kushirikiana na baadhi ya viongozi kukihujumu chama hicho,”amesema mmoja wa wajumbe hao.

Maganza amesema halmashauri hiyo imemteua Riziki Ngaga (Mwenyekiti wa wanawake mkoa wa Dar es Salaam) kuwa katibu Mkuu mpya wa TLP.

Alipoulizwa kuhusiana Ofisi ya Msajili kutokuwa na taarifa na mkutano huo, amesema ulikuwa halali na makamu mwenyekiti wa chama hicho alipeleka barua.

“Ukitaka kujua mkutano ulikuwa halali naendelea kupokea pongezi mbalimbali kutoka kwa watu, na ule mkutano kulikuwa na viashiria vya uvunjifu wa ikatulazimu kuomba ulinzi wa polisi,”amesema Maganza.

Lyimo ambaye Ofisi ya Msajili inamtambua ndiye katibu mkuu, alipotafutwa azungumzie hilo, hakuwa tayari kuzungumza akitaka atafutwe kesho Jumatatu.


ADC nayo yapata viongozi wapya

Katika uchaguzi wa ADC, viongozi wapya waliopatikana ni Mwenyekiti Taifa, Shabani Haji Itutu ambaye aliibuka kidedea dhidi ya Doyo Hassan Doyo.

Uchaguzi mkuu huo wa nne wa ADC ulifanyika katika ukumbi Lamada, baada ya viongozi kumaliza muda wao wa kipindi cha miaka 10, kwa mujibu wa katiba, akiwemo mwenyekiti Hamad Rashid Mohamed.

Aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo Mwalimu Hamad Azizi alisema kati ya kura 192 zilizopigwa, Itutu alipata kura 121 dhidi ya Doyo aliyepata kura 70 na moja iliharibika.

Kwa upande wa makamu mwenyekiti Zanzibar, Azizi alisema kati ya wagombea waliokuwa wakigombea nafasi hiyo, Fatuma Salehe alipata kura 120 dhidi ya Shara Amran aliyepata kura 49 na nne ziliharibika.

 “Kwa makamu mwenyekiti Bara Hassan Mvungi alipata kura 135 dhidi ya Scola Kahana aliyepata kura 35 ambapo kura tatu zimeharibika na kubainisha kuwa kura 19 hazikupigwa na wajumbea.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Itutu, alisema nafasi ya katibu mkuu na manaibu wake upande wa Bara na Zanzibar zitatangazwa katika mkutano na waandishi wa habari.