Mshtakiwa alia kusota rumande tangu 2015

Mshtakiwa, Abubakar Kasanga anayekabiliwa na shtaka la mauaji akipelekwa mahabusu baada ya kusomewa shtaka lake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Pamela Chilongola
Muktasari:
- Mshtakiwa Abubakar Kasanga amedai kuwa yupo rumande tangu mwaka 2015 na anaumwa hapati matibabu kwa wakati.
Dar es Salaam. Mshtakiwa Abubakar Kasanga anayekabiliwa na kesi ya mauaji ameieza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa yupo rumande tangu mwaka 2015, hivyo ameiomba mahakama hiyo iharakishe shauri hilo ili liweze kwenda mbele.
Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa kati ya Oktoba 24, 2014 katika nyumba ya kulala wageni ya Musoma iliyopo eneo la Maguruwe wilaya ya Temeke alimuua Amina Abdallah.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali, Cuthbert Mbilingi kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa jalada la shauri hilo linaandaliwa taarifa kwa ajili ya kwenda Mahakama Kuu ili mshtakiwa aweze kusomewa maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo.
Mshtakiwa Kasanga alidai kuwa shauri hilo lipo tangu mwaka 2015 na lilisomwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Mei 3, 2015 na ilipofika Novemba 7, 2019 ilihamishiwa Mahakama Kuu.
Alidai shauri hilo liliondolewa Mahakama Kuu na kurudishiwa mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa madai upelelezi haukukamilika baada ya kukamilika Desemba 2019 ilihamishiwa Mahakama Kuu.
"Shauri hili liliondolewa na kurudishwa polisi kwa ajili ya mahojiliano, ambapo mwaka 2020 kesi ilirudishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na imesikilizwa mashahidi wawili tu tangu mwaka 2015, hivyo naiomba mahakama hii iharakishe shauri hili kwa kuwa ni mgonjwa sipati matibabu kwa muda," alidai mshtakiwa huyo.
Baada ya maelezo hayo, ndipo Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ferdnadri Kihwonde alipoutaka upande wa mashtaka kuandaa hati mpya ya mashtaka kwa ajili ya kwenda Mahakama Kuu ili mshtakiwa huyo aweze kusomewa maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Agosti 21, 2023 kwa ajili ya kutajwa.