Mshtakiwa kesi ya waliyokuwa vigogo NIC afariki dunia

Muktasari:
- Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 365, yakiwemo ya kughushi nyaraka, kutakatisha fedha, kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa, kichepusha fedha, kuongoza genge la uhalifu na kusababishia hasara ya Sh 1.8bil shirika la NIC.
Dar es Salaam. Mshtakiwa Mwaforo Ngereja, aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya kuchepusha fedha na kuisabishia hasara ya Sh1.8 bilioni za Shirika la Bima la Taifa (NIC), amefariki dunia.
Marehemu Ngereja na wezake saba, akiwemo aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Sam Kamanga wanakabiliwa na mashtaka 365 yakiwemo ya kughushi, kutakatisha fedha, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kuongoza genge la uhalifu, kuchepusha fedha na kusabaishia hasara NIC.
Wakili wa Serikali Mkuu, Ladslaus Komanya akishirikiana na Timothy Mmari na Blandina Mnung'a ameeleza hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Januari 23, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo (commital proceedings).
Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa shauri hilo umekamilika na washtakiwa wanatakiwa kusomewa hayo, ili kesi ianze kusikilizwa.
Akitoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, Komanya alidai upande wa mashtaka walipewa taarifa na mdhamini wa Mafworo ambaye ni Jamal Ngereja, kuwa mshtakiwa huyo amefariki dunia Januari 4, 2024 wilayani Kilosa.
Komanya alidai Ngereja amewasilisha mahakamani hapo barua ya kuitaarifu mahakama kuhusiana na kifo hicho, huku akiambatanisha na kibali cha maziko.
Amedai Januari 6, 2024, mwili wa Mafworo ulisafirishwa kutoka Kilosa kwenda Segerema mkoani Geita kwa ajili ya maziko.
"Mheshimwa hakimu kutokana na taarifa hii, tunaomba mahakama itupe ahirisho fupi la kesi hii ili tuweze kujiridhisha kwa mamlaka nyingine kuhusiana na taarifa za kifo hiki," amedai Wakili Komanya.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Swallo alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 26, 2024.
Mbali na Kamanga na Mafworo, washtakiwa wengine ni Tabu Kingu ambaye alikuwa kaimu mhasibu mkuu wa shirika hilo, Victor Mleleu na Peter Nzunda ambao walikuwa wahasibu wa shirika hilo.
Washtakiwa wengine ni Kenan Mpalanguro; Lusubilo Sambo na Eshimendi Uronu.
Hata hivyo, mshtakiwa Maleleu, Nzunda, Mparanguro na Sambo wanaendelea kubaki rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria, huku mshtakiwa Kamanga, Kingu na Uronu wakiwa nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba Mahakama Kuu.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka hayo 365, ambayo yapo ya kughushi nyaraka za uongo, kutakatisha fedha, kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa, kichepusha fedha, kuongoza genge la uhalifu na kulisababishia hasara Shirika hilo ya Sh 1.8bilioni.
Washtakiwa hao wanadaiwa katika shtaka la kuongoza genge la uhalifu wanadaiwa walitenda kosa hilo kati ya Januari Mosi 2013 na Desemba 31, 2018 katika maeneo tofauti tofauti jijini Dar es Salaam, mkoani Rukwa, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Morogoro na Kigoma.