Msimamo tofauti wa Mbowe, Lissu mjadala

Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiendelea na operesheni +255 Katiba Mpya katika Kanda ya Kaskazini, kauli kinzani zimeibuka kati ya viongozi wa juu wa chama hicho -- mwenyekiti Freeman Mbowe na makamu wake, Tundu Lissu.

Viongozi hao wanaoongoza timu mbili zinazoshiriki operesheni hiyo wamekuwa na kauli tofautikuhusu suala la maridhiano baina ya chama hicho, Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kutofautiana huko kumeibua mijadala ndani na nje ya chama na kuwaacha baadhi ya wanachama wasijue la kufanya.

“Unajua maridhiano yana faida, hata hii mikutano ya hadhara ambayo Lissu anaitumia kusema maridhiano hayajaonyesha matokeo, msingi wake ni maridhiano, wanachama wetu wenye kesi mbalimbali wameachiwa, kesi zenyewe za Lissu zimefutwa,” alisema kiongozi mmoja wa kamati kuu ya chama hicho.

“Hata ruzuku tumechukua msingi wake ni maridhiano. Ni kweli yawezekana kuna mambo hajaridhika, ila maridhiano yameonesha matokeo makubwa.”

Wakati kigogo huyo akieleza hayo, aliyewahi kuwa mbunge kupitia chama hicho aliyeomba jina lihifadhiwe alisema “maridhiano haya yanaturudisha nyuma sisi. Yanatufanya tuonekana kama tumesalimu amri, ni bora tuendelee na ujenzi wa chama, hawa tunaoridhiana nao si wa kuwaamini sana.”

Hata hivyo, Mbowe kwenye moja ya mikutano wa hadhara ya operesheni +255 mkoani Kigoma alisema wanaodai yeye (Mbowe) na Lissu hawaelewani wanakosea, hilo halipo na wanaendelea kuchapa kazi kama kawaida.

Mbowe akieleza hayo na kusisitiza kuwa maridhiano yataendelea, Lissu katika mikutano anayoongoza yeye Kigoma na Katavi amekuwa akikosoa mambo mbalimbali yanayoendelea, akisisitiza kuwa “maridhiano ya kweli ni kupatikana kwa Katiba mpya.”

Awali, akiwa Singida, katika mwendelezo wa mikutano yake ya hadhara, Lissu alisema, “kuna maneno mengi ya upatanisho, lakini maridhiano pekee ni upatikanaji wa Katiba mpya, tusipokuwa na Katiba mpya tumeliwa. Maridhiano ambayo hayana ukweli, watu waliumizwa sana lakini hawajaambiwa kwa nini waliumizwa, wala nani aliyeamuru waumizwe wala kufidiwa,” alisema.

Alipoulizwa jana, Lissu alisema mikutano ya hadhara imeruhusiwa kutokana na shinikizo la ndani na nje ya nchi kwa serikali ya Samia na wafungwa wa kisiasa na kesi za kubambikiza vivyo hivyo, pia hata

Mbowe hakuachiliwa kwa sababu ya maridhiano bali kwa presha kubwa ndani na nje ya nchi.

“Kesi ilishabuma. Rais Samia hakuwa na jinsi bali kukubaliana na shinikizo hilo,” alisema.

Alisema yale yote yanayohitaji mabadiliko ya sera, sheria na katiba (kwenye maridhiano) hayajatekelezwa hata moja na mchakato wa Katiba Mpya haujaanza lakini muda hautusubiri.

Alisema hata yake ambayo hayahitaji mabadiliko yoyote ya kisheria au kisera, kama vile kuwaondoa wabunge 1p wa viti maalumu ambao Chadema iliwafukuza uanachama Rais Samia ameshindwa au kukataa kuyafanya.

Hata hivyo, alisema “sio sahihi kusema hatuoni kilichofanyika. Tunaona kilichofanyika, lakini sio kwa sababu zinazopigiwa chapuo.”

Mbowe hakupatikana jana kuzungumzia utofauti huo, lakini akizungumza wakati wa uzinduzi wa Operesheni +255 Katiba Mpya Mei 17, 2023, bila kuweka wazi alisema katika taasisi yoyote kutokuelewana hakukosekani.

Alisema pamoja na kuwepo changamoto hiyo, viongozi wa chama hicho wanaendeleza mapigano ya kuhakikisha Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi vinapatikana.

“Natambua kuna watu wanasema viongozi wa Chadema tuna kutoelewana, hiyo ni kawaida kwani hata vikombe vikiwa kabatini lazima vigongane ndivyo ilivyo, hata sehemu yenye watu wengi hapakosi migogoro, lakini niwahakikishie tunaendelea na maridhiano ili kuhakikisha Watanzania wanapatiwa Katiba Mpya,” alisema Mbowe

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na gazeti hili, wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya kauli hizo za Mbowe na Lissu kuhusu maridhiano, wakisema mapito waliyopita viongozi hao yanatofautiana, ndiyo maana hicho kinatokea.


Maridhiano vs harakati

Mchambuzi wa siasa, Rainery Songea alisema kupishana kauli viongozi kupo, lakini mwishowe kitakachoangaliwa ni msimamo wa chama chao.

Alisema Mbowe anaweza kuwa na maoni yake, vivyo hivyo Lissu, lakini ukiangalia msimamo wa Chadema inaunga mkono maridhiano.

“Kimsingi, pamoja na kupishana lakini kuna vitu wanakubaliana,” alisema.

“Ukimuangalia Mbowe na Lissu ni watu wanaopishana kidogo kimtizamo; Mbowe anaamini katika maridhiano, ila Lissu anaamini zaidi katika harakati, hii ndiyo tofauti yao,” alisema.

“Sasa wakipishana hivi, jambo kubwa linalopaswa kuangaliwa ni msimamo wa chama ukoje, yaani kamati kuu,” aliongeza.

Hata hivyo, Songea alisema ukiangalia kwa jicho la mbali zaidi, Mbowe na Lissu wanakubaliana na maridhiano, shida iliyopo ni mitizamo tu.

Ukiacha hali hiyo, Songea alisema maridhiano yameanza kuzaa matunda, kama vile watu kuandamana kwa ulinzi wa polisi.

Suala la matunda ya maridhiano pia linatazamwa na Dk Faraja Kristomus, msomi wa Sayansi ya Siasa, anayesema “maridhiano kati ya Rais Samia na Chadema yameleta matunda, ikiwemo kuondoa mikwamo mbalimbali ya kisiasa iliyowekwa kwa miaka mitano.”

Kwa upande wake Gabriel Mwang’onda, mchambuzi wa siasa na uchumi, alisema Chadema ni chama kikubwa kwa sasa na hivyo kutofautiana kimtazamo baina ya viongozi ni jambo la kawaida.

Hata hivyo, alisema inaogopesha pale mitazamo inavyotofautiana mbele ya umma.

“Hawa ni binadamu, wanaweza wakawa na mitizamo tofauti, lakini hii mitizamo si kwamba wanatofautiana sana, wote wana lengo moja, isipokuwa namna ya kufikisha ujumbe wao ndiyo tofauti.

“Mara kadhaa Mbowe amekuwa akisisitiza hajalambishwa asali na kwamba harakati zao za mapambano hazififishwi na maridhiano. Lakini Lissu pamoja na kutoelezea, fursa ya kufanya mikutano ya hadhara au kurejea nchini ni matunda ya mazungumzo,” alisema Mwang’onda.

Alisema alichokifanya Rais Samia na Mbowe ni kitu cha kupigiwa mfano na anaamini anachokifanya Lissu ni jambo la kawaida na ajenda za kisiasa ili kuonekana uwepo wake na kuhoji masuala yaliyojitokeza miaka mitano iliyopita.

“Inasaidia kutisha ili hayo yasitokee tena, kujenga uelewa kwa Watanzania kwamba haya yaliyotokea miaka mitano iliyopita yalikuwa na madhila mabaya na hayatakiwi kujirudia. Kukiri kwa Serikali kumeshafanyika, nadhani umesikia ile kamwe…tusirudi tulikotoka,” alisema.

Mwang’onda alisema huwezi kumzuia mtu kuzungumza, hasa Lissu ambaye madhila yaliyomtokea ni tofauti na Mbowe. Alisema Lissu alijeruhiwa kwa risasi, wakati Mbowe alifungwa jela sambamba na kuharibiwa biashara zake.

“Hatuwezi kupima uchungu wa Lissu, maana ilikuwa kufa au kupona, acha atoe ya moyoni ili kupata ahueni zaidi. Si kwamba Mbowe hakuathiriwa, tena alipata changamoto ndani ya utawala huu pia,” alisema Mwang’onda.


Hatua za maridhiano, faida zake

Majadiliano ya kwanza ya maridhiano yalifanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma Mei 20, mwaka jana ambapo Rais Samia akiambatana na viongozi waandamizi wa CCM na Serikali walikutana na ujumbe wa viongozi wa Chadema ulioongozwa na Mbowe.

Kikao kingine cha faragha kilifanyika Novemba 5, 2022 jijini Dar es Salaam na vigogo wa CCM wakiongozwa na makamu mwenyekiti (Bara), Abdulrahman Kinana na upande wa Chadema uliongozwa na Mbowe.

Moja ya mafanikio ya mazungumzo hayo, Rais Samia alihudhuria na kuhutubia kongamano la Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) lililofanyika Machi 8, mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Akihutubia kongamano hilo, alisema maridhiano waliyoanza hayatawaacha salama kwa sababu kuna wahafidhina kwenye vyama ambao hawataridhika.

Rais Samia alisema utamaduni wa kukaa chini na kuzungumza si jambo rahisi kwa watu wengi na unakuwa na vikwazo kwa pande zote za mazungumzo.

“Kwa hiyo mwenyekiti (Mbowe), wahafidhina wapo kwangu na kwako pia,” alisema Rais Samia.

Jambo jingine kubwa la maridhiano linalotajwa ni kuwa Godbless Lema, mbunge wa zamani wa Arusha Mjini aliyekuwa akiishi uhamishoni Canada tangu mwaka 2020 kutokana na hofu ya kutishiwa maisha yake naye amerejea Tanzania.

Vivyo hivyo, mikutano ya hadhara imerejea huku mchakato wa Katiba mpya ukifanyiwa kazi na Serikali ilitangaza kuongeza takribani Sh9 bilioni katika bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ya mwaka 2023/24.

Maridhiano hayo kwa namna moja au nyingine, yamesababisha Chadema kuchukua fedha za ruzuku walizokuwa wamesusia tangu mwaka 2020, kwa kile walichodai hawakukubaliana na matokeo ya uchaguzi mkuu.

Mei 11 wanawake wa Bawacha walifanya maandamano ya kushinikiza Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuwaondoa wabunge 19 waliofukuzwa uanachama na kupoteza sifa ya kuwa wabunge ambayo yalilindwa na jeshi la polisi, jambo ambalo huko nyuma lisingewezekana.