Mbowe atoa sharti kujiunga Chadema, Lissu alilia stahiki zake

Kigoma. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewaonya watu wanaojiunga na chama hicho kwa lengo la kupata vyeo huku akiwataka watetea haki na usawa kwa wananchi.

Mbowe alitoa onyo hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Kasulu Mjini mkoani Kigoma jana na kuongeza kuwa, ili uwe mwanachama lazima uamini katika misingi minne hasa haki.

Alitaja misingi mingine inayotakiwa kusimamiwa na kiongozi wa chama hicho kuwa ni kuwekeza katika maendeleo ya watu, kuongoza kwa kuzingatia uhuru, demokrasia na maendeleo ya watu.

“Ni marufuku kuingia Chadema ili upate cheo, unaingia kupigani haki kwa watu wote. Kama unaamini katika haki, uhuru, demokrasia na maendeleo ya watu wote hiki ndio chama sahihi kwako, pia usiingie Chadema kwa sababu unampenda Mbowe wala rangi ya bendera,” alisema.

“Mbowe anaweza kwenda mbele za haki kesho, kwa hiyo kama unakuja Chadema kwa sababu yake utapotea lakini kama lengo ni kulinda imani dhidi ya haki, uhuru, demokrasia na maendeleo ya watu, ni sehemu sahihi kwako.”

Kiongozi huyo alitoa wito kwa viongozi na wanachama wa vyama vingine vya siasa nchini wanaoamini katika misingi hiyo kujiunga Chadema kwa kile alichodai lengo ni kukiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani.

“Hatupaswi kugombania fito tunajenga nyumba moja, tunawaomba wana mageuzi wanaojitambua na wenye imani imara njooni tujenge chama imara, tuiondoe CCM madarakani.

“Tulikuwa na vyama vitano hadi sita vyenye nguvu nchini, lakini vingine vilishindwa ile mikikimikiki, vikaunga juhudi za Serikali ya CCM. Kuna wana Chadema waliopewa fedha na vyeo wakasaliti imani lakini Kasulu mlisimamia imani ndiyo maana ninazungumza hapa leo (jana).”

Mbowe aliwataka wananchi kujipanga ili kufanikisha uundwaji wa Katiba Mpya itakayofanikisha misingi hiyo kutekelezwa kwa vitendo na Tume Huru ya Uchaguzi itakayosaidia kuwapata viongozi watakaosimamia misingi ya chama hicho.

“Tumepita maeneo mengi ya Mkoa wa Kigoma kila sehemu ni malalamiko, wengine wanalalamika kuvunjiwa vibanda vyao, kutolipwa fidia kwenye maeneo yaliyopitiwa na miradi, ardhi yao kutwaliwa bila kufuata sheria. Lakini haya hayatipatiwa mwarobaini kwa Katiba iliyopo,” alisema Mbowe.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu aliitaka Serikali kutoa ruhusa kwa Zanzibar na Tanganyika kuchagua aina ya muungano wanaouaka huku akikosoa uliopo.

Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Kitanga (NCCR Mageuzi), Ayubu Nyambere alipopatiwa nafasi ya kuhutubia katika mkutano huo alikitaka chama hicho kuendelea kuelimisha umma kuhusu hali ya siasa nchini aliyodai imeimarika.

Wakati Mbowe akiwa Kasulu Mjini, Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu alikuwa Kasulu Vijijini akisema watu wanafikiria yeye na Rais Samia Suluhu Hassan mambo yao yako vizuri lakini hana uhakika kwa sababu hajalipwa stahiki zake.

Septemba 7, 2017 Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana katika makazi yake eneo la Area D jijini Dodoma muda mchache baada ya kutoka bungeni.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Kasulu Vijijini, Lissu alisema baada ya kushambuliwa kwa risasi kipindi alichokuwa mbunge, aliuguzwa kwa michango ya wananchi na watu wengine sehemu mbalimbali duniani kwa miaka mitatu.

Alisema sheria ya Bunge imeweka wazi mbunge anayeumwa anapaswa kulipiwa gharama za matibabu yeye pamoja na mtu atakayemsindikiza iwe ndani au nje ya nchi.

“...Rais Samia alipokuja Ubelgiji nilimwambia ulipokuja Nairobi kuniona uliona nilivyokuwa nimechakazwa na sasa wewe hutaki kunilipia matibabu, akaniambia nimuandikie,” alisema Lissu.

Alisema ameamua kuweka suala hilo hadharani kwa kuwa, kumekuwa na taarifa za uongo uongo, kuwa kila mbunge anayetumikia akimaliza muda wake hulipwa kiinua mgongo.

“Kuna fedha nilitakiwa kulipwa, nimelipwa sehemu ikapelekwa benki kwa kuwa nilikuwa nimekopa nyingine iliyobaki bado naisubiri,” alisema.

Pia, alidai kuwa picha zilizosambazwa kwenye mabango ni za kudanganya watu kuwa mambo ni mazuri lakini mambo sio mazuri huku akisisitiza watu wasipewe imani potofu.

Uamuzi wa Lissu kusema hayo, ulitokana na risala iliyosomwa na wananchi, wakieleza changamoto zinazowakabili wakimtaka kiongozi huyo kuzifikishia kwa Rais Samia.

Akizungumzia changamoto za wananchi alisema, yapo mambo mawili yanayoleta shida ikiwamo hifadhi za misitu na haki za ardhi za wananchi.

Alisema tatizo hilo ni kubwa kwa nchi nzima, kwa kuwa maofisa wa wanyamapori na misitu wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi.