Prime
Msimamo wa KKKT kwa Samia

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) pamoja na Waumini wa Kanisa hilo kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa hilo yaliyofanyika Makumira mkoani Arusha.
Dar/Arusha. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limeweka wazi msimamo wake kuhusu utendaji wa Serikali Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono uwekezaji.
Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Frederick Shoo amesema wana imani na Rais huyo kwa namna anavyofanyia kazi hoja mbalimbali wanazowasilisha kwake na hivyo wataendelea kushauri, kukosoa na kukemea pale inapobidi.
Hata hivyo, alitoa angaliwa kuwa itakapobidi kukemea wasiambiwe wanachanganya dini na siasa.
Hoja ya Askofu Shoo imekuja siku moja baada ya kauli iliyotolewa juzi na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete katika hafla ya ufunguzi wa Kanisa la Waadventisti Wasabato mkoani Mara, kuwa viongozi wa dini hawapaswi kuchanganya dini na siasa; na kuwa wanasiasa nao wasitumie dini kwa masilahi yao binafsi.
“Kama kuna viongozi wa dini wanaotaka kutuelekeza kuitumia dini kwa manufaa ya kisiasa na kama kuna viongozi wa siasa wanataka kuitumia dini kwa manufaa yao ya kisiasa nawaombeni tuwanyanyapae,” alisema Kikwete.
Askofu Shoo alitoa kauli hiyo jijini Arusha jana, alipohutubia hafla ya maadhimisho ya miaka 60 ya kuanzishwa kwa KKKT, ambayo Rais Samia alikuwa mgeni rasmi.
Akijenga hoja hiyo, Askofu Shoo alisema ni wajibu wa viongozi wa dini kuwaombea viongozi wa umma, kuwashauri na ikibidi kuwakemea.
Alisema ni kazi ya viongozi wa dini kuwaombea viongozi wa Serikali ili watimize wajibu wao vema na wanapoona kuna mahali hapajaenda sawa hawataacha kuwashauri.
“Kama kuna mahali pa kukemea tutakemea pia na hapa ndipo ninaposema ikifika kwenye hatua hiyo tusiambiwe msichanganye dini na siasa,” alisema kiongozi huyo ambaye pia ni askofu wa Dayosisi ya Kaskazini.
Katika hotuba yake hiyo, Askofu Shoo aliisifu hatua ya Rais Samia kukaa kimya dhidi ya kauli kutoka kwa taasisi na wananchi mbalimbali kuhusu mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji na uboreshaji wa bandari nchini, kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai.
“Lipo hili la DP World kwanza naomba ieleweke wazi kwamba kanisa linaunga mkono uwekezaji, hatupingi uwekezaji na tunajua wewe kwenye nia yako unataka wawekezaji, hata hivyo jambo hili limekuwa na maoni mbalimbali ya wananchi na vyombo vya habari, viongozi wa dini zote, kwenye mitandao tumeona maoni mbalimbali.
“Nashukuru Mungu amekujalia hekima kama mama na kiongozi umekaa kimya, lakini kimya chako hicho si kwamba hufanyii kazi, mimi nasema jambo hili linahitaji hekima kubwa ya kuliendelea na sisi tunakuombea kwa Mungu ili hekima yote itumike kuliendea jambo hili ili muafaka upatikane,” alisema.
“Hata hivyo, tunatambua kwamba sisi viongozi wa dini zote kwa uwakilishi, tuliomba kuja kukuona pale mwanzoni kabisa mwa jambo hili.
“Kwa uungwana wako na unyenyekevu na utayari wa kusikiliza, ulitupokea na tulikuletea maoni yetu kama taasisi na viongozi wakuu wa dini, madhehebu yote, tukiwa CCT (Jumuiya ya Kikristo Tanzania), TEC (Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania), Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania) mimi nakumbuka jinsi ulivyotupokea,” alisema akisisitiza kuwa maoni yao yalipokewa.
Hakuna mwenye misuli
Akizungumzia suala la ukimya wake kwenye sakata hilo, Rais Samia amesema aliamua kukaa kimya na ataendelea kufanya hivyo.
“Niliamua kunyamaza kimya na naendelea kunyamaza kimya, ninachotaka kuwahakikishia, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa Taifa hili. Hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuuza Taifa hili, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuharibu amani na usalama tuliojenga kwenye Taifa hili. Sasa hayo itoshe kuwa ni ujumbe wangu kwenu,” alisema Rais Samia.
Asifu uongozi wake
Katika hatua nyingine, Askofu Shoo alisema pamoja na mazingira magumu aliyopokea kijiti cha urais, Rais Samia ametengeneza historia yake.
Samia aliapishwa kuwa Rais Machi 19 mwaka 2021 baada ya kifo cha Rais John Magufuli Machi 17 mwaka huo.
Askofu Shoo alisema wengine hawakuamini na wapo wasiotaka uongozi wake na hadi sasa wamebaki na jinamizi hilo.
“Nakuomba ufanye kazi yako kwa kujiamini na ufanye kazi yako kwa ujasiri na ujue, sisi tuliosoma alama za nyakati, naomba nikwambie Mungu ndiye amekuweka kwenye nafasi hiyo na hilo tunaliheshimu,” alisema Askofu Shoo.
Alimsifu mkuu huyo wa nchi kwa kudumisha amani, upendo mshikamano na kukuza uhuru wa kuongea, diplomasia ya uchumi, demokrasia ya vyama vingi na alimtaka aendelee nayo.
Alieleza pia kufurahishwa na falsafa ya kujenga uchumi kwa kutegemea sekta binafsi.
“Kanisa la KKKT tulipotoa waraka wakati ule tulipata shida kwelikweli, moja ya mambo tuliyozungumza ni ushirikishwaji wa sekta binafsi, hii sasa falsafa ya kujenga uchumi kwa kutegemea sekta binafsi ili kukuza uchumi, ajira na kipato cha Watanzania,” alisema.
Rais Samia alitumia sehemu ya hotuba yake, kuwashukuru viongozi wa dini akiwemo Askofu Shoo na Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza kwa ushauri wao wa kuanzisha jumuiya ya mariadhiano Tanzania ambayo imekua na tija kwa Taifa.
Tatizo la kodi
Miongoni mwa mambo mengi aliyozungumzia Askofu Shoo, ni kero za baadhi ya kodi zinazotozwa hasa katika maeneo ya huduma za wananchi kwenye miradi ya kanisa.
Alitolea mfano uwepo wa vituo vya kulea watoto wenye matatizo ya kuona, vinavyotaka kupigwa mnada kwa sababu ya madeni, akisema kuna haja ya kupata msaada wa Rais.
Vilevile, alilalamikia kodi ya ardhi katika taasisi za elimu akisema maeneo mengine yanakuwa ni ya uzalishaji wa chakula cha wanafunzi lakini Wizara ya Ardhi inakwenda kudai kodi.
Askofu Shoo, pia alizungumzia hospitali teule za wilaya ambazo Serikali ilikuwa imeziteua kuwa za wilaya, sasa imeachana nazo baada ya kujenga za kwake huku ikiondoa watumishi wake.
“Unawaondoa watumishi wote, taasisi hizi zimehudumia wananchi karibu miaka 60. Ni kama mama ameshakunyonyesha, tangu udogo, mama ameisha nguvu, umepata nguvu za kurukaruka kidogo unakuja unamng’ata kwenye ziwa, acheni,”
Akijibu suala la kodi kwenye hotuba yake, Rais Samia alisema Serikali inatambua mchango wa taasisi za dini katika utoaji wa huduma za afya, elimu, uwezeshwaji wananchi kiuchumi na utoaji wa huduma shufaa na itaendelea kushirikiana ili wananchi wapate huduma stahiki.
"Kuhusu changamoto zote ulizozisema mkuu wa kanisa ninakuahidi nitazifanyia kazi na zinazojitokeza na zitakazoendelea kujitokeza ili sera ya kitaifa ya ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi (PPP) iendelee kuwatumikia wananchi," alisema.
Vilevile, Rais Samia aligusia maadili akiwaomba viongozi wa dini kwa kushirikiana na Serikali kukuza, kusimamia na kuenzi maadili mema hasa kwa vijana kwa kuzingatia mila, desturi ili Taifa liwe na maadili mema.
"Katika kukuza, kusimamia na kuenzi maadili yetu, itakuwepo kazi ya kanisa na Serikali kuwajengea maadili vijana ili waje kuwa na maadili mema na kutunza Taifa letu na kazi hii inatakiwa kuanza kwenye malezi ya watoto na vijana," alisema.
Kauli ya Bakwata
Akitoa salamu katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma alisema ni jukumu la viongozi wa dini kuishauri, kushirikiana na kuungana na Serikali katika kuiombea nchi na viongozi wake.
Baraza hilo, alisema limekuwa likishirikiana na makanisa mbalimbali katika shughuli zake, katika ile kaulimbiu ya ‘dini mbalimbali umoja na amani’. "Sisi viongozi wa dini tutaendelea kuiombea nchi yetu na kuendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo," alisema Mruma akimwakilisha Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir