Prime
Msongamano wa malori Dar shida, suluhu ipo hapa-3
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, ukuaji wa shughuli za bandari usioendana na upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji mizigo, ni miongoni mwa mizizi ya tatizo hilo
Dar es Salaam. Wakati bandari kavu zikitupiwa lawama kama sababu ya msongamano wa malori jijini Dar es Salaam, wadau wa sekta hiyo wanasema tatizo ni zaidi ya bandari hizo na suluhisho lake linahitaji ushirikiano wa pande kadhaa.
Kwa mujibu wa wadau hao, ukuaji wa shughuli za bandari usioendana na upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji mizigo, ni miongoni mwa mizizi ya tatizo hilo.
Hata hivyo, Serikali mkoani humo, inasema tayari imeunda kamati maalumu kushughulikia tatizo la msongamano wa malori.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Bandari Kavu Tanzania (CIDAT), Meleck Shange anasema changamoto hiyo inatokana na ukuaji wa shughuli za bandari ambao haujaenda sambamba na upanuzi wa miundombinu ya nje ya bandari.
Bandari kavu zimekuwa zikipokea lawama nyingi kutoka kwa wananchi kuhusu foleni za malori, lakini anasema sehemu kubwa ya changamoto hiyo inatokana na uwezo mdogo wa miundombinu ya usafiri ikilinganishwa na mahitaji ya sasa.
Anasema Serikali tayari imeanza kushughulikia suala hilo kupitia timu maalumu iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kwa lengo la kutafuta suluhisho la kudumu la msongamano wa malori jijini.
“Tunaamini suluhisho litapatikana. Serikali imeonesha utayari wa kusikiliza na kutafuta njia za kupunguza msongamano huu,” anasema.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa kupunguza msongamano wa malori barabarani, Shange anasema waendeshaji wa bandari kavu huweka wasimamizi wa usafiri (traffic marshals) katika maeneo ya kuingilia na kutoka ili kuhakikisha magari yanaingia kwa utaratibu na barabara zinaendelea kupitika.
Anasema pia baadhi ya madereva hupewa ratiba nyingine za kufika kuchukua mizigo au kurudisha makontena pale uwezo wa kuhudumia magari unapokuwa umefikiwa, ili kuzuia malori mengi kujikusanya kwa wakati mmoja.
“Tunapogundua msongamano ni mkubwa tunaweka wasimamizi wa trafiki kusaidia kufungua njia na kuhakikisha shughuli nyingine za kijamii haziathiriki. Wakati mwingine madereva huombwa kuahirisha safari zao na kufika siku inayofuata kulingana na ukubwa wa mzigo unaohudumiwa kwa wakati huo,” anasema.
Shange anasema baadhi ya changamoto husababishwa na madereva wanaosubiri kupata kazi karibu na maeneo ya bandari kavu, jambo ambalo huongeza idadi ya malori yanayoegeshwa kandokando ya barabara.
Anasema pale madereva wanaposhindwa kufuata maelekezo, huwashirikisha askari wa Jeshi la Polisi kusaidia kurejesha utaratibu na kufungua njia kwa watumiaji wengine wa barabara.
Kuhusu Bandari Kavu ya Kwala iliyojengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa mizigo Dar es Salaam, Shange anasema kituo hicho kina nafasi muhimu katika kuhudumia mizigo ya transit inayokwenda nchi jirani, lakini hakiwezi kubeba mzigo wote unaobaki ndani ya Dar es Salaam.
Anasema takribani asilimia 80 ya mizigo inayoshushwa bandarini hubaki Dar es Salaam, huku asilimia 20 pekee ikisafirishwa kwenda mikoa mingine au nchi jirani.
“Ni vigumu kupeleka mizigo yote Kwala wakati walaji wengi wako Dar es Salaam. Kufanya hivyo kungeongeza gharama na safari za malori kurudi tena mjini,” anasema.
Idadi ya bandari kavu yaongezeka
Shange anasema kwa sasa kuna vituo 16 vya kuhifadhi magari yanayoingizwa nchini, zaidi ya vituo 21 vya kuhifadhi makontena yenye mizigo, vituo vinane vya makontena matupu na zaidi ya vituo 58 vya huduma za usafirishaji wa bidhaa za kuuza nje ya nchi (CFS).
Amesema mahitaji yanavyoendelea kuongezeka, ndivyo uwekezaji katika bandari kavu unavyoongezeka katika maeneo mbalimbali ikiwamo Mlandizi, Morogoro, Dodoma na Isaka.
Madereva watupiwa mpira
Shange anasema sehemu ya msongamano unaoonekana katika baadhi ya maeneo ya bandari kavu hausababishwi moja kwa moja na shughuli za upakuaji au upokeaji mizigo, bali na madereva wa malori wanaokusanyika karibu na vituo hivyo wakisubiri kupata zabuni au kazi za kusafirisha mizigo.
Anasema madereva wengi huamini kuwa uwepo karibu na bandari kavu huongeza nafasi ya kupata mteja kwa haraka, jambo linalochangia kuongezeka kwa idadi ya malori yanayoegeshwa kandokando ya barabara na katika maeneo ya huduma.
“Wengi wanakuwa wanasubiri kupata kazi. Dereva anaamini akikaa karibu na bandari kavu anaweza kumpata mteja anayehitaji huduma ya usafirishaji. Hili ni moja ya sababu zinazochangia kuonekana kwa malori mengi katika maeneo hayo,” anasema.
Anasema ongezeko la mizigo bandarini limechochea uwekezaji mkubwa katika sekta ya usafirishaji, huku idadi ya malori ikiongezeka kwa kasi kuliko uwezo wa miundombinu na maeneo rasmi ya maegesho kuyahudumia.
Kikosi usalama barabarani
Akizungumza Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, William Mkonda anasema kuna kamati imeundwa kwa ajili ya kushughulikia jambo hilo.
“Tayari kuna kamati imeundwa kwa ajili ya kushughulikia jambo hilo hivyo tusubiri,” anasema Mkonda.
Mipango Miji
Mmoja wa maofisa wa Idara ya Mipango Miji katika Jiji la Dar es Salaam anasema wakati bandari kavu zilipoanza, haikutarajiwa idadi ya malori na shughuli za usafirishaji ingeongezeka kwa kasi kiasi cha kuathiri maeneo ya makazi na kusababisha msongamano mkubwa wa magari pamoja na malalamiko kutoka kwa wananchi.
Anasema kutokana na hali hiyo, mamlaka zimekuwa makini zaidi katika utoaji wa vibali vipya vya uwekezaji wa shughuli zinazohusiana na uhifadhi na usafirishaji wa mizigo, huku baadhi ya maombi yakisitishwa hadi hapo maeneo stahiki yatakapopatikana na miundombinu kuendana na mahitaji yaliyopo.
“Lengo ni kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinaendelea bila kuathiri makazi ya wananchi, huduma za kijamii na matumizi mengine ya ardhi,”anasema.
Anasema sheria za mipango miji za mwaka 2007 na kanuni zake za mwaka 2028 zinatoa nafasi kwa wananchi watakaokuwa tayari kuuza maeneo yao ili kupisha uwekezaji unaokidhi vigezo vya matumizi ya ardhi, lakini hatua hiyo lazima ifuate taratibu zote za kisheria.
Anasema kabla ya eneo kubadilishwa matumizi kutoka makazi kwenda biashara au shughuli za viwanda na usafirishaji, ni lazima kutolewa tangazo rasmi la mabadiliko ya matumizi ya ardhi ili kutoa fursa kwa wadau na wananchi kutoa maoni yao kabla ya uamuzi wa mwisho kufanyika.