Mto Ruaha wakauka siku 130

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa mto Ruaha Mkuu umekauka kwa takribani siku 130 na kusababisha madhara kwa wanyama katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kutokana na shughuli za kibinadamu kando ya mto huo.

Iringa. Imeelezwa kuwa mto Ruaha Mkuu umekauka kwa takribani siku 130 na kusababisha madhara kwa wanyama katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kutokana na shughuli za kibinadamu kando ya mto huo.

Hayo yameelezwa leo Desemba 19, 2022 na Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Godwell Ole Meinga’ataki katika kongamano la wanahabari na wadau wa uhifadhi, mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji linalofanyika mkoani Iringa.

Katika kongamano hilo lililoandaliwa na kituo cha wanahabari watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA), Meinga’ataki amesema kukauka kwa mto huo kumesababisha wanyama kufa kwa kukosa maji na mlipuko wa ugonjwa ya kimeta.

“Maji yakikauka mto huwa unabaki na vidibwi vidogo ambavyo samaki wanakufa kwa wingi kutokana na maji hayo kujaa matope na kinyesi cha wanyama yanakuwa hayana Oksijeni ya kutosha kwa ajili ya viumbe wanaotegemea kuishi majini hivyo unakuta viumbe wengi wanakufa.

“Mto Ruaha Mkuu ndio uhai wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa sababu ndio chanzo cha maji kwa wanyama,uoto wa asili unaosababishwa na maji na mito mingine inayoingiza maji katika mto Ruaha hususani bonde la mto Usangu,” amesema Meinga’ataki

Amesema kuwa kukauka kwa mto Ruaha kumesababishwa na shughuli za kilimo na ufugaji ndani ya hifadhi ya bonde la Usangu na kilimo kando ya vyanzo vya maji ambavyo vinapeleka maji hayo katika bonde la Ihefu na Usangu.

“Umuhimu wa kuhifadhi mto Ruaha na vyanzo vyake sio tu muhimu kwa ajili ya hifadhi ya Ruaha lakini ni muhimu kwa ajili ya suala la uzalishaji wa umeme Mtera Kidatu na sasa katika mradi mkubwa wa Nyerere”.


Amesema kuna wananchi wengine wanaotegemea mto Ruaha kwa ajili ya shuguli za kilimo na ufugaji na matumizi ya nyumbani mto ukiwa hauna maji hata shughuli za kibinadamu hazitafanyika.


“Tunawaomba wakulima na wafugaji kuzingatia matumizi bora ya maji pia kumekuwa na changamoto ya mifugo mingi ambayo inaingia eneo la maji katika hilo bonde na kuleta madhara namaji kutawanyika sana naa kukosa kurudi katika uelekeo”