Mto Ruvuma watajwa chanzo tembo kuvamia Newala

Mtwara. Kupungua kwa maji ya Mto Ruvuma, kunatajwa kusababisha tembo na wanyama wengine kuvamia maeneo jirani na mto huo ikiwamo Wilaya ya Newala mkoani Mtwara.

Hayo yamebainishwa leo Jumapili Oktoba 29, 2023 na Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini Mashariki, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa), Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Abraham Jullu.

 “Yaani hatujawahi kupata taarifa yoyote kuhusu tembo kuwepo Newala wala Masasi tulipofika tulibaini kuwa Mto Ruvuma unaotenganisha nchi ya Msumbiji na Tanzania umepungukiwa na maji hivyo tembo wanapita kutokana na kuwepo kwa maji madogo,”amesema Kamanda Jullu

“Huu ni msimu wa korosho tembo wanafata mabibo wanapenda hata tulipowafata tuliwakuta shambani kwenye mikorosho hata wengi waliojeruhiwa walikutwa shambani” amesema Kamanda Jullu

“Tatizo hili ni kubwa kwenye kanda hii nguvukazi yetu kuwepo kwenye maeneo yote inakuwa ni ngumu kwakuwa tulijua kuwa kuna salama na hatukuweka nguvu  hali ambayo sasa inatulazimu kwenda kutoa elimu huko” amesema Kamanda Jullu

Naye Ismail Mussa mkazi wa Mchori Godauni amesema kuwa amejeruhiwa na tembo akiwa analinda korosho shambani majira ya usiku ambpo nikiwa huko nilivamiwa na tembo na kujeruhiwa.

“Nilikuwa nyumbani nikatoka saa mbili usiku kwenda shambani kulinda korosho nikiwa shambani nilivamiwa na tembo hakunijeruhi sana nilikuwa peke yangu lakini kwa sasa naendelea vizuri,” amesema Mussa

Mkuu wa Wilaya ya Newala, Mwangi Kundya amesema kuwa kutokana na tembo wawili kuonekana kuwa na hasira waliuwawa ili kupunguza madhara.

“Tulipata tabu baada ya tembo kuonekana karibu na hospitali ya wilaya, asubuhi hawakuonekana hii ilitupa kiwewe sana ambapo tulilazimika kuwatafuta mpaka tulipowapata,”amesema.