Wahanga 54 wa tembo walipwa fidia Kiteto

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Kimana akiangalia uharibifu wa mazao yake uliofanywa na tembo. Picha na Mohamed Hamad
Kiteto. Serikali imelipa kifuta machozi watu 54 waliopata madhara ya wanyama wakali aina ya tembo waliotoka hifadhini na kuvamia makazi kisha kuharibu mazao shambani na hata kuua watu.
Akizungumzia madhara ya tembo, Lazaro linjano, Afisa maliasili kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kiteto, amesema Serikali inatambua madhara yatokanayo na wanyama hao wakali aina ya tembo.
"Serikali inatambua madhara yatokanayo na wanyamapori wakali aina ya tembo ambao wafanya uharibifu, Wizara ya Maliasili na Utalii (WMU), iliandaa mwongozo mwaka 2012 kwa ajili ya kutoa kifuta machozi kwa wahanga husika ,"amesema Linjano
Amesema Halmashauri ya Kiteto imeendelea kutoa elimu kwa ajili ya utekelezaji wa kanuni hizo ambapo kuanzia mwaka 2021 wananchi waliendelea kulipwa kifuta machozi na Wizara ya Maliasili na Utalii.
"Serikali kupitia Wizara ya maliasili na Utalii imekuwa ikilipa kifuta machozi wahanga, wanaopata madhara ambapo hujaza fomu na kuituma Wizarani kwa ajili ya malipo"amesema
Amesema mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imewalipa wahanga 54 kati ya hao 3 walifariki na 51 ni waathirika kwenye mazao na mifugo yao
Kuhusu kukabiliana na wanyama hao wasilete madhara zaidi kwa wananchi Linjano amesema wamekuwa wakitoa elimu ya namna ya kuwadhibiti kwa kupiga kelele kutumia vuvuzela, madebe na kifaa kinachotoa kelele kali ambayo wanyama hao hawapendi kusikia
"Tunawashauri wananchi kujenga vihenge imara na wavune mazao yao mara yanapokuwa tayari pamoja na kukaa umbali wa mita 50 walipo tembo hao,"amesisitiza Linjano