Sh700 milioni zatolewa kwa vikundi Mbeya, wafujaji mikopo waonywa

Muktasari:
- Mkopo huo umetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na kukabidhiwa na Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza leo Ijumaa Julai 4, 2025 huku vikundi 32 vimenufaika.
Mbeya. Vikundi 32 vya wajasiriamali, maofisa usafirishaji na wakulima Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wamenufaika na mkopo wa zaidi ya Sh700 milioni kutoka halmashauri ya wilaya ikiwa ni sehemu ya asilimia 10, huku tahadhari ikitolewa kwa wale wenye tabia ya kutumia mikopo kinyume kilichopangwa.
Mkopo huo umekabidhiwa leo Ijumaa Julai 4, 2025 na Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza katika hafla fupi iliyofanyika katika Stendi ya Tarafani katika Mji mdogo wa Mbalizi, Wilaya ya Mbeya.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mbeya Vijijini, Beatrice Ngutu amewataka wanufaika kwenda kuitumia vizuri fedha walizopata kuinua uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.
Ofisa Tarafa Kata ya Isangati, Aron Sote amesema wako baadhi ya watu wakipata pesa huzitumia kwa mambo yasiyo ya msingi, lakini wameweka mikakati watakaobainika watachukiwa hatua.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya, Akimu Mwalupindi amesema wanaipongeza Serikali kwa hatua ya kuwezesha makundi hayo kujikwamua kiuchumi.
Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mbeya, Agness Elkunda amesema vikundi 32 vimesajiliwa na kunufaika na mkopo asilimia 10.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitano sasa halmashauri imetoa mikopo isiyo na riba ya zaidi ya Sh4.5 bilioni kwa makundi mbalimbali.
Mmoja wa wanufaika Jane Amos ameomba Serikali kuwa na utaratibu wa kuhamasisha vikundi kulipa kwa wakati ili kuepuka vikwazo katika makusanyo.