Mtoto wa miaka mitatu adaiwa kuchinjwa, akutwa ndani ya kiroba

Muktasari:
- Mtoto wa miaka mitatu wilayani Newala auwawa kikatili kwa kuchinjwa na kuwekwa kwenye mfuko wa kiroba.
Mtwara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linamshikilia mtu mmoja kwa tukio la kumchinja mtoto (3) kwa kumtoa koromeo na kusababisha kifo chake katika Kijiji cha Lichingu wilayani Newala.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP-Mtaki Kurwijila amesema kuwa tukio hilo lilitokea saa 11 jioni katika Kijiji cha Lichingu ambapo mtuhumiwa aitwae Osward Dadi (35) amekamatwa kwa tuhuma za kumuua mtoto Nazareti Abdulahman (3) kwa kumchinja kisha kumuweka kwenye mfuko wa kiroba (shangazi kaja).
Kamanda amesema kuwa mtoto huyo alikuwa akicheza na wenzake nyumba ya jirani na anapoishi mtuhumiwa ambapo alimwita ndani huku akiwaacha watoto wengine wakiendelea kucheza nje.
Mtuhumiwa alifanikiwa kumkata koromeo na kusababisha damu nyingi kutoka hivyo kupelekea umauti wa mtoto huyo.
Kamanda mama wa mtoto alianza kumtafuta mtoto wake na kuambiwa kuwa yuko ndani kwenye nyumba ya mtuhumiwa.
Aidha wananchi wenye hasira kali walimjeruhi mtuhumiwa kwa kumshambulia kisha kupelekwa hospitalini na amesema baada ya kupata nafuu watafanya naye mahojiano.
Amina Mandova (mama wa mtoto) amesema kuwa kitendo hicho kimefanyika kwa muda mfupi ambapo kitendo cha kuingia ndani na kufunga mlango alirudi na kukuta mtoto wake hayupo.
“Yaani ilikuwa muda mfupi sana alikuwa anacheza na wenzie kwenye michanga hapa mbele ya nyumba nilitoka kidogo nikasema ngoja niende kumfata sikumkuta nilipomuulizia kwa mwenzie nikaambiwa yuko na ndani kwa ozward nilipomuita hakuitikia,” amesema.
“Yaani nikamuita Ozward, akatoka nje akiwa na mifuko kama anataka kusafiri nikashangaa Ozward namuita haongei yuko kimya ikabidi nimuite baba wa mtoto ili kupata msaada na watu wengine walifika na kufanikiwa kunyang’anya mfuko ambapo baada ya kuumimina tulibaini kuwa na kisu chenye damu nyingi na vikorokoro vingine kwa kweli nilipoona kisu kina damu nilianza kulia, sijawahi kuwa na mazoea na Ozward kabisa,” amesema Mandova.
Ashura Mohamed ambaye ni jirani amesema kuwa mtuhumiwa anaishi nyumba ya pili kutoka kwake ambapo huwa hapendi mazoea na watu na pia anatuhumiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja hivyo wanaomfuata pale ni wale marafiki zake.
“Yaani alitumia dakika chache hata tano hazikufika kufanya kitendo hicho cha mauaji, yaani mtoto alikuwa hapo na tulimuona kufumba na kufumbua hayupo hata kilio chake hatukusikia inasikitisha sana,” amesema.
Mtuhumiwa hakuwa mtu wa watu, alipenda kujitenga ana marafiki wanakuja kumtembelea ambapo anaishi peke yake hata tukio lilifanyika akiwa peke yake,” amesema.
Mkazi wa eneo hilo, Zainabu Saambili amesema kuwa hawa watoto wote wawili alikuwa nao ndani aliwapa chakula wakala waliposhiba wakatoka kucheza mbele ya nyumba yao.
“Nikiwa ndani nimekaa nikasikia mtoto akilia nje kwa muda mfupi kukawa kimya wakati najiandaa kwenda kuwasikiliza nikasikia mama yake anamwita Naa, nikatoka nje tulipouliza tukaambiwa yuko ndani kwa Ozward wakati tunamuuliza alijifanya chizi,” amesema.
Mwenyekiti wa Mtaa Dadi Kubanga amesema tukio hili llimetokea jana jioni, baada ya kupata taarifa tulikuta mazingira siyo mazuri na nilikuta mtuhumiwa akipigwa nje nyumba anayoishi.
“Mtuhumiwa aliwahi kuishi Newala ambapo mtaa alioishi alipotea mzee mmoja mwezi Mei mwaka huu hawajazika na hajulikani alipo mpaka sasa, lakini mwezi wa nane mwaka huu mtoto alinusurika kutekwa majira ya saa moja kasoro usiku," amesema Kubanga.
Kaimu Mganga Mfawidhi Hosptilia ya Halmashauri ya Newala Mji Dr Kideyi Mzelela amekili kupokea watu wawili mmoja akiwa majeruhi na mwingine akiwa amefariki.
"Jana saa moja usiku tulipokea mwili wa mtoto mmoja ambaye tulidhibitisha kifo chake na kumuhifadhi ambapo tulimfanyia uchunguzi na ilikubaini chanzo cha kifo chake ambapo alikuwa na jeraha shingoni sehemu ya koromeo ndiyo chanzo cha kifo chake ambapo hakuna kiungo ambacho kilitolewa.