Mufti ataja mchango wa Mzee Mwinyi Bakwata

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubaar Zubeir akizungumza katka dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi

Muktasari:

Dua hiyo imefanyika katika Msikiti wa Mohamed wa sita Kinondoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulrahaman Kinana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu.


Dar es Salaam. Baraza la Waislamu Tanzania Bakwata limefanya dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi,  huku likieleza mchango alioutoa kwa taasisi hiyo.

Dua hiyo imefanyika katika Msikiti wa Mohamed wa sita Kinondoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulrahaman Kinana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu.

Mzee Mwinyi alifariki Dunia Februari 29 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam na kuzikwa Machi 2, kijijini kwake Mangapwani, Zanzibar.

Akizungumza leo Jumatatu Machi 11, 2024 Mufti wa Tanzania,  Sheikh Abubakar Zubeir amesema wakati wa uongozi wake, Bakwata iliweka utaratibu wa mabadiliko ya katiba yake.

Amesema awali kulikuwa na Sheikh Mkuu wa Tanzania baada ya mabadiliko hayo mwaka 1985 kukawa na Mufti ambaye ndio Sheikh Mkuu.

 "Kwenye Baraza la Maulid lililofanyika Songea mkoani Ruvuma, Rais Mwinyi alikuwa mgeni rasmi na ndiye aliyemvalisha Mufti joho," amesema Sheikh Zubeir.

Mufti amesema katika utawala wa Mzee Mwinyi alianzisha utaratibu wa kuswali katika misikiti tofauti tofauti wakati wa mwezi wa Ramadhani.

"Jambo hilo ni kubwa linaonyesha unyenyekevu na moyo wa kujali, alikuwa ni mwepesi wa kusikiliza watu," amesema.

Jambo lingine alilofanya Mzee Mwinyi kwa mujibu wa Mufti,  wakati wa uongozi wake aliwezesha safari za kwenda Hijja, tofauti na kipindi cha nyuma ambapo palikuwa na  ugumu kutokana na upatikanaji wa fedha za kigeni lakini yeye akalifanya kuwa jepesi.

"Jambo lingine ni mageuzi ya kihistoria mwaka 1993 kwenye sekta ya elimu ambapo ulifanyika mkutano na kuhudhuriwa na Mzee Mwinyi, amefanya makubwa sio kwa Serikali tu hata kwa taasisi yetu," amesema.

Kwa upande wake,  Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Abdulrahaman Kinana, amesema Mzee Mwinyi alikuwa na sifa zote za uongozi zilizopo kwenye vitabu vya dini.

Amesema mtu anapozingatia maagizo ya Mungu anakuwa kwenye nafasi ya kuongoza wengine.

"Sifa zote zilizozungumzwa ni muhimu sana mtu anapaswa kuwa msikivu, muungwana na mkarimu kama alivyokuwa mzee wetu Mwinyi yote yaliyoelezwa alizingatia tabia na maagizo ya Mwenyezi Mungu," amesema Kinana.

Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuiga tabia ya Mzee Mwinyi kwenye mambo yote ikiwemo kielimu, kijamii, kisiasa na hata kitamaduni.

Kwa upande wake, Salum Mwalimu amesema Mwinyi alikuwa ni mtu wa kujishusha,  hivyo viongozi hasa vijana wanapaswa kujifunza.

Amebainisha kuwa viongozi wa Kiislamu, walikuwa wakiona kujiweka wazi ni ushamba, lakini kupitia uongozi wa Mzee Mwinyi hilo liliwezekana.

 "Mzee wetu alikuwa ni mkweli na muwazi, alifundisha watu kuwa majasiri kujituma na kufanya kazi kwa bidii," amesema Mwalimu.