Muliro aanza na uhalifu, 15 mbaroni

Muliro aanza na uhalifu, 15 mbaroni

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa 15 kwa tuhuma za wizi wa kutumia silaha na pikipiki, uvamizi nyakati za usiku na uporaji.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa 15 kwa tuhuma za wizi wa kutumia silaha na pikipiki, uvamizi nyakati za usiku na uporaji.

Watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni inayoendelea, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro aliyoyatoa Juni 8 na akitaka kufanyike kwa operesheni hiyo kwa mwezi mmoja.

Akizungumza jana, kamanda wa kanda hiyo, Muliro Jumanne alisema jeshi hilo linamshikilia Edson Boniface (24) mkazi wa Kimara na wenzake tisa wakituhumiwa kutumia pikipiki, kupita mitaani na maeneo yenye miamala ya pesa ili kuvizia wateja wanaochukua pesa na kuwafuatilia nyuma kisha kuwapora.

Alisema wahalifu wengine wamekuwa wakipokea mali za wizi, zilizoibiwa ikiwamo vifaa vya ujenzi kwenye miradi mbalimbali lakini majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.

Pia, alisema katika operesheni hiyo, walifanikiwa kumkamata Mohamed Mussa (Kibosile) kwa tuhuma za kughushi nyaraka za Serikali na zisizo za Serikali kwa kutumia mihuri na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu. “Mtuhumiwa huyu alikamatwa na vifaa ikiwamo mihuri tofauti 24, vyeti vya kuhitimu sekondari, vyeti vya masomo ya sekondi, vyeti vya hati za tabia njema za Jeshi la Polisi na vibali vya uraia kwa wageni,” alisema.