Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Museveni asimulia alivyoruka kihunzi mchele wa Tanzania

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex leo Januari 12,2024.

Muktasari:

  • Rais Museveni amesimulia kisa cha kale alichokiita dhambi nne cha kupiga marufuku Uganda kuagiza mchele kutoka Tanzania.

Dar/Zanzibar. Rais Yoweri Museveni wa Uganda, ameeleza alivyoruka kihunzi cha shinikizo la kusitisha vibali vya kuagiza mchele kutoka Tanzania, huku akitaja sababu nne zilizochagiza asipige marufuku hiyo.

 Hatua ya Museveni kutakiwa kupiga marufuku uingizaji wa mchele wa Tanzania katika nchi yake, ilitokana na kile alichoarifiwa kuwa, bidhaa hiyo imeua watu kadhaa wa Uganda.

Hata hivyo, mkuu huyo wa nchi amesema alikataa kupiga marufuku bidhaa hiyo kwa kuwa yeye si kipofu na kwamba, angefanya hivyo Tanzania na Uganda zingeingia katika kile alichokiita mchezo wa kitoto, yaani kulipizana kisasi.

Museveni ametoa kauli hiyo leo Januari 12,2024 alipopewa nafasi ya kutoa salamu za Uganda katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizofanyika katika Uwanja wa New Amaan.

“Nyuma kule Uganda waliniambia kwamba mpunga wa Tanzania umetuua huku Uganda, walikuwa wanataka nipige marufuku mchele wa Tanzania, nikasema siwezi kufanya hivyo, mimi si kipofu,” amesema.

Iwapo angetekeleza hatua ya kupiga marufuku mchele huo, Museveni alisema angelifanya kile alichokiita dhambi nne.

Alizifafanua dhambi hizo kuwa ni kuingia katika mchezo wa kitoto wa kulipizana kisasi kati yake na Tanzania kwa kila nchi kuamua kupiga marufuku uingizaji bidhaa za mwenzake.

“Nikifanya hivyo Serikali ya Tanzania nayo italipiza kisasi wanapiga marufuku hiki, mimi napiga marufuku kile, mchezo wa watoto siwezi kufanya namna hiyo,” amesema.

Dhambi nyingine amesema ni kulazimisha Waganda wanunue mchele wa bei ya juu ili kuwatetea wavivu wasiolima kuleta ushindani wa uzalishaji.

Ameeleza kufanya hivyo kungesababisha vikwazo kwa Tanzania ambayo imefikia hatua nzuri ya kilimo cha zao hilo, badala ya kuihamasisha.

“Badala ya kum-encourage (kumhamasisha) nampiga kwenye kichwa, hii ni mbaya sana,” amesema.

Kwa mujibu wa Museveni, kufanya hivyo kungesababisha baadhi ya wakulima wa mpunga nchini Uganda kuendelea kubweteka kwa kuwa hawatapata shinikizo kutoka kwa mshindani.

Kuhusu mapinduzi, Museveni amesema Serikali ya hayati Abeid Amani Karume (Rais wa Kwanza wa Zanzibar) ilikuwa na fikra iliyofanana na Uganda ya kuungana na Tanganyika.

Hata hivyo, ameeleza mafanikio ya muungano huo ni matokeo ya juhudi kubwa za wanamajumui wa Afrika.

“Sisi tunakubali na tunaamini kwamba, Afrika haiwezi kuendelea bila kuungana. Tumekuwa na mvutano kati ya watu wa aina mbili yaani wanamapinduzi na wale wengine,” amesema.

Ameeleza kushangazwa na wanaopinga muungano akisema ama ni vipofu au wanyonyaji.

“Ama ni vipofu au ni wanyonyaji kwa sababu mimi ni mzalishajimali niko na shida ya soko, huwezi kuniambia mambo ya kujitengatenga kwa sababu nifanye mambo yangu,” amesema.


Rais Samia

Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, akizungumza katika maadhimisho hayo amesema miaka 60 ya mapinduzi ndiyo mwanzo wa safari, akiahidi kutengeneza mazingira yatakayorahisisha uzuri wa safari hiyo zaidi.

Awali, Rais Samia alichapisha ujumbe kuhusu sherehe hizo katika kurasa za mitandao yake ya kijamii akiandika, miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar yamefanyika mageuzi makubwa ya kimaendeleo, ikiwamo uboreshaji wa sekta ya afya.

“Sote ni mashahidi wa hatua hizi. Shuhuda mojawapo ni ufunguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi - Lumumba, Zanzibar. Mwaka 1976 nilikuwa mwanafunzi katika Shule ya Lumumba Zanzibar.

“Wakati huo, eneo ilipojengwa hospitali hii mpya ya kisasa palikuwa na zahanati ndogo kabisa iliyoitwa Miwanzini. Kutoka zahanati ile ndogo hadi hapa tulipo leo ni hatua kubwa na ya kujivunia.”

Kupitia ujumbe huo, Rais Samia amesema maendeleo ni hatua, jasho na damu na suala endelevu, hivyo kuwataka Wazanzibari kuendelea kuwashukuru, kuwapongeza, na kuwaombea dua waasisi ambao waliweka misingi ya kufika hatua hiyo.

“Jukumu sasa kwa kila mmoja wetu ni kutambua tulipotoka, malengo yetu kama Taifa na kuendelea kufanya kazi kila mmoja kwa nafasi yake ili kupiga hatua kubwa zaidi, huku tukibaki kuwa wamoja, wenye amani na utulivu,” amesema.


Rais Kagame

Kwa upande wake, Rais wa Rwanda, Paul Kagame aliwapongeza Wazanzibari kuendeleza malengo na matarajio ya waasisi.

"Muungano huu unaleta ushahidi kwamba Afrika tupo pamoja katika kushughulikia matatizo yetu wenyewe, hakuna kisichowezekana tunapotembea pamoja,” amesema.

Kagame amesema: “Hongereni sana na tumedumu sana katika mapinduzi kwa hiyo tunaweza kuungana kama ndugu kama Taifa."

Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, amesema mataifa hayo yanaendelea kushirikiana katika kuleta maendeleo ya nchi hizo za Afrika Mashariki.

Naye, Waziri Mkuu wa Burundi, Gervais Ndirakobuca amesema Taifa hilo halitasahau jinsi Tanzania ilivyowasaidia walipopata matatizo na kuomba udugu huo uendele kudumishwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema zilitumika siku 22 tangu Desemba 20, mwaka jana za kufungua miradi na kuweka mawe ya msingi kabla ya kufikia kilele cha maadhimisho jana.

"Tutaendelea kuyalinda, kuyaenzi na kuyadumisha mapinduzi haya maana yametuunganisha kutoka katika manyanyaso ya mkoloni na leo yametuletea maendeleo makubwa," amesema.

Hemed amesema Serikali zote zitaendelea kuwaunga mkono Rais Samia na Dk Mwinyi.

Viongozi wengine wa kitaifa waliohudhuria sherehe hizo ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko; maspika Dk Tulia Ackson na Zubeir Maulid; majaji wakuu, Profesa Ibrahim Juma na Khamis Ramadhan Abdallah; na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud.

Kwa upande wa viongozi wastaafu waliohudhuria ni Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na mawaziri wakuu, Mizengo Pinda na Frederick Sumaye.


Ilivyokuwa uwanjani

Viongozi mbalimbali wa kitaifa na wananchi walianza kuwasili uwanja wa New Amaan Complex, milango ya kuingia uwanjani ilifunguliwa kuanzia saa nne asubuhi.

Wananchi walipata fursa ya kuingia muda huo, huku wageni waalikwa walianza kuingia saa saba mchana wakifuatiwa na viongozi wakuu wastaafu na wa sasa.

Rais Mwinyi aliingia uwanjani saa 10.10 jioni akiwa katika gari la wazi, akizunguka uwanja kuwasalimu viongozi na wananchi waliojitokeza kwa wingi katika sherehe hizo.

Baada ya kushuka kwenye gari, ilipigwa mizinga 21, kuimbwa wimbo wa Taifa wa Zanzibar na wimbo maalumu wa mashujaa.

Alikagua gwaride kabla ya kupanda jukwaani kuketi.

Baada ya kupanda jukwaani kiongozi huyo wa Taifa, alipokea maandamano ya vikundi mbalimbali vya wananchi, vyuo vya elimu na taasisi za Serikali vikiwa na mabango yaliyokuwa yameandikwa ujumbe tofauti kuhusu mapinduzi.

Gwaride la kijeshi lilipita mbele yake kwa mwendo wa pole na wa haraka.

Maonyesho ya zana na silaha zinazotumiwa na majeshi ilikuwa kivutio kikubwa kwa wananchi waliohudhuria sherehe hizo.

Yalihusisha helikopta mbili zilizoonyesha jinsi ya kuokoa askari aliyetekwa.

Mbele ya Rais yalipita magari ya silaha kubwa za kivita.

Katika sherehe hizo, waliozaliwa Januari 12, 1964 ambao walitimiza miaka 60 jana, walirusha maputo na njiwa uwanjani hapo, shughuli iliyoambatana na wimbo maalumu wa miaka 60 ya mapinduzi.

Vikundi maalumu vya kijeshi vilionyesha kazi zao za wanamaji na nchi kavu, huku askari wakiwa wamebeba mabegi mazito.