Mvua yaleta madhara Dar
Muktasari:
- Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, zimeleta kizazaa, huku watu wakihama makazi yao kupisha maji yapungue.
Dar es Salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, zimesababisha nyumba zilizopo Mtaa wa Califonia, Kata ya Kagera, wilayani Kinodndoni, kujaa maji na wakazi wa eneo hilo kulazimika kuhama makazi yao kwa muda.
Mvua hizo katika maeneo mengi jijini humo zimeanza saa 11:30 alfajiri ya leo Desemba 8, 2023 ambapo wakazi wa eneo hilo wamesema walianza kuona maji yanaingia kwenye nyumba zao saa 1:30 asubuhi.
“Nilianza kuona maji yanaingia ndani kama saa 1:30 asubuhi, lakini mvua ilianza tangu alfajiri, nilitoka nje kujiokoa, mpaka hapa tunapozungumza maji yamejaa kwenye nyumba hadi madirishani hivyo sijafanikiwa kuokoa chochote,”amesema Hassan Ally mkazi wa eneo hilo.
Amesema aliona ni muhimu uhai kuliko kung’ang’ana kutoa vitu ambavyo vinanunuliwa.
"Tupo hapa tunasubiri maji yapungue ili tuangalie kitu kipi ambacho ni kizima, kwa mvua ile iliyokuwa inanyesha kwa nguvu nilijua ingeweza kuleta athari hii," amesema Ally.