Mwakilishi Mkazi UNDP ataja urasimu unawakatisha tamaa wanawake kuomba kazi

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Dk Christine Musisi akizungumza katika Jukwaa la The Citizen Rising Woman, linalofanyika katika ukumbi wa The Dome, jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Mwakilishi Mkazi wa UNDP, ataka kuwepo kwa washauri au watu wa kuwaongoza wanawake katika taasisi au makampuni.
Dar es Salaam. Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Dk Christine Musisi amesema wanawake wengi katika nchi zinazoendelea wamekuwa waoga kuomba kazi kutokana na mazingira ya urasimu yaliyopo katika taasisi.Amesema hali hiyo inatokana na kutokuwa na watu ambao ni waongozaji katika kampuni kuanzia anapoingia katika kampuni au taasisi hadi anapokuja kuwa na nafasi kubwa katika uongozi.Dk Musisi amesema hayo leo, Machi 8, 2023 katika Mdahalo wa Siku ya Wanawake Duniani ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kupitia mradi wa Rising Woman unaoendeshwa na Gazeti la The Citizen.Mradi wa Rising Woman ni maalumu kwa ajili ya kutambua mchango wa wanawake katika maeneo yao ya kazi waliofanya vizuri ili kuwahamasisha mabinti na wanawake wengine ufanya vizuri katika kazi zao.Amesema ili kukabiliana na hali hiyo, ni vizuri kuwepo kwa waongozaji au washauri katika taasisi au kampuni kwani hiyo itakuwa ni njia ya kumwezesha mwanawake na kumwandaa kuwa kiongozi bora."Tatizo kubwa lililopo katika nchi zinazoendelea ni kwamba wanawake wengi hawapati nafasi za kusogea mbele na hili linatokana na hofu yao katika kuomba kazi, hivyo tunaweza kuwa na mentalship katika mashiriki au taasisi zetu ili wanawake waweze kuandaliwa na kuwa viongozi bora," amesema Dk Musisi na kuongeza"Lakini kuna wakati wanawake tunawekwa katika mazingira tunashindwa kuzungumza maana inaweza kutokea unataka kuelezea jambo unaonekana umepata hisia kali," amesema.Hii ni mara ya tatu kwa Gazeti la The Citizen kuandaa mradi huo wa Rising Woman, kwa mara ya kwanza ulianza mwaka 2020.
Hata hivyo, kauli mbinu ya siku hiyo ya Wanawake Duniani kwa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd ni uwezeshwaji wanawake katika ngazi ya uongozi