Mwanafunzi aliyemjeruhi mwalimu kwa panga kichwani asota mahabusu

Muktasari:

Afya ya mwalimu aliyejeruhiwa kwa panga na mwanafunzi wake ikiwa inaimarika, huku mwanafunzi akiendelea kusota rumande.

Sengerema. Wakati afya ya mwalimu Stanford Mgaya Shule ya Sekondari Tamabu iliyoko Wilayani Sengerema, Mkoa wa mwanza ikiendelea kuimarika, mwanafunzi Alex Butawantemi (18) anayedaiwa kumjeruhi mwalimu huyo, anaendelea kusota mahabusu ya polisi mkoani Mwanza siku ya nane pasipo kufikishwa mahakamani. 

Mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari Tamabu wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza anatuhumiwa kumjeruhi mwalimu huyo, Septemba 25, 2023 mwaka huu maeneo mbalimbali ya mwili wake kwa kutumia panga.

Akizungumuza na Mwananchi kwa njia ya simu mke wa mwalimu huyo Margareth Maberi amesema hali ya mume wake inaendelea kuimarika siku hadi siku ingawa ikifika majira ya jioni kichwa kinamuuma na leo walikuwa hospitali kwa ajili ya kuendelea na matibabu kisha kurudi nyumbani.

"Nawashukuru madaktari wote waliomuhudumia mume wangu kutokana na hali yake kuendelea kuimarika,” amesema Maberi.

Mke alipoulizwa juu ya mumewe kama anaweza kuzungumza na waandishi wa habari, amesema kutokana na kuumwa kichwa ameshauriwa na madaktari kuwa asipokee simu hadi hali yake itakapoimarika zaidi.

Septemba 25, 2023 mwalimu Mgaya wa Shule ya Sekondari Tamabu alijeruhiwa kwa panga kichwani na mkono na mwanafunzi wake Alex Butawantemi (18) anayesoma kidato cha tatu shuleni wakati mwalimu huyo alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kila siku.

Hali iliyopelekea mwanafunzi huyo kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi ambapo hadi sasa bado yuko rumande akisubili hatima yake ya kwenda mahakamani au la, huku wadau mbalimbali wa elimu wakilaani kitendo hicho na kutaka mwanafunzi huyo apewe adhabu inayostahili.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Tamabu, Emmanuel Gerevazi amesema walimu wa shule yake wako vizuri wanaendelea na kuchapa kazi na shule imetulia huku wanafunzi wakiendelea kusoma ili kufikia malengo yao.

Wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wakuu wa shule 42 za Sekondari Halmashauri ya Sengerema wamesema walimu wa Tamabu sekondari wanatakiwa wasivunjike moyo waendelee kufanya ili watoto wanaowafundisha wafikie malengo yao.