Mwanafunzi kidato cha sita amjeruhi mwalimu kwa chepe kichwani

Muktasari:

  •  Ni wa Shule ya Sekondari Mwika iliyopo wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Moshi. Mwanafunzi wa kiume wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Mwika, wilayani hapa mkoani Kilimanjaro amempiga mwalimu wake kwa kutumia chepe kichwani na kumsababishia majeraha.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Machi 25, 2024 wakati mwalimu huyo aliyetambulika kwa jina moja la Matendo, alipokuwa akizunguka kukagua wanafunzi waliokuwa wanajisomea usiku.

Inadaiwa alipokuwa akifanya ukaguzi alivamiwa na mwanafunzi huyo aliyemjeruhi kisha kutoroka shuleni hapo.

Ofisa Elimu Mkoa wa Kilimanjaro, Jimmy Nkwamu, amesema taarifa za tukio hilo amezipata na jana Machi 26, 2024 alimtuma ofisa elimu wilaya kwenda kufuatilia shuleni hapo kujua ni nini hasa kilitokea.

"Nilimtuma jana Ofisa Elimu Wilaya (DEO) kwa niaba yangu aende shuleni, lakini bado hajaniletea taarifa. Naomba nifuatilie, hivi sasa siwezi kuzungumza chochote juu ya tukio hilo maana sijaletewa taarifa," amesema.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kuzungumzia tukio hilo, ameomba apewe muda kulifuatilia ili aweze kulitolea taarifa sahihi.

"Niko barabarani, ngoja nifuatilie nitakupa taarifa sahihi," amesema Kamanda Maigwa.

Mkuu wa shule hiyo, Damiano Gwaltu amesema taarifa ya tukio walishapeleka kwenye mamlaka husika hivyo  hawezi kulizungumzia akitaka watafutwe viongozi wa elimu ngazi ya wilaya na mkoa.

"Nipo kwenye semina na suala hili limeshaenda kwa ofisa elimu wilaya na mkoa, sitaweza kulitolea taarifa kwa kuwa limeshazifikia mamlaka hizo, naomba uwasiliane na uongozi kuipata taarifa hii," amesema.

Mwananchi Digital ilimtafuta mwalimu aliyejeruhiwa ambaye amemtaka amesema,  "naomba ujaribu kufuata taratibu za kiuongozi, ukifuata mtiririko wa uongozi taarifa itakuwa nzuri zaidi kuliko kupitia moja kwa moja kwangu. Hilo litakuwa jambo jema zaidi, maana kuna uongozi wa shule, bodi ya shule, ofisa elimu wilaya na mkoa; ukifuata hizo taratibu itakuwa ni jambo zuri kwamba nipo radhi nieleze kwa sababu wao ndio wanaotoa maelekezo," amesema.