Mwanamuziki wa Nigeria kortini kwa kuishi Tanzania kinyemela

Mshtakiwa Daniel Imah akiwa chini ya ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo Aprili 6, 2024.

Muktasari:

  • Iman anadaiwa kutenda kosa hilo, Aprili 3, 2024 eneo la Kigamboni

Dar es Salaam. Raia wa Nigeria, Daniel Imah (29) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na shtaka la kuwepo nchini Tanzania kinyume cha sheria.

 Mshtakiwa ambaye ni mwanamuziki, amefikishwa mahakamani hapo leo, Aprili 8, 2024 na kusomewa shtaka na wakili wa Serikali, Hadija Masoud, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga.

Akimsomea shtaka lake, wakili Masoud amedai Aprili 3, 2024 katika eneo la Kigamboni katika Ofisi za Uhamiaji zilizopo Wilaya ya Kigamboni, mshtakiwa akiwa raia wa Nigeria alipatikana akiishi nchini bila kuwa na kibali wala nyaraka inayoonyesha uhalali wa kuishi nchini. Mshtakiwa alikana kutenda kosa lake.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo kuomba tarehe kwa ajili ya kumsomea hoja za awali (PH).

Hata hivyo, Hakimu Ruboroga alimuuliza mshtakiwa kwa nini yupo nchini kinyume cha sheria, naye alidai alikuja nchini kwa rafiki yake na malengo yake yalikuwa kwenda nchini Poland kusoma. Seehemu ya mahojiani yalikuwa kama ifuatavyo.

Hakimu: Umekuja lini nchini?

Mshtakiwa: Nilikuja Tanzania tangu Oktoba 2023, rafiki yangu aliniita nikaja nikawa nakaa naye.

Hakimu: Ulikuwa unakaa naye wapi?

Mshtakiwa: Nilifikia Kariakoo, lakini baadaye kutoka na kuwa na kelele pale nilihamia Mbezi Beach. Baada ya kukaa kule Mbezi Beach, nilihamia Kigamboni ambapo huyo rafiki yangu alinipangia chumba kimoja.

Hakimu: Kwa muda wote ulikuwa unafanyaje?

Mshtakiwa: Nilikuwa nasubiria kugongewa muhuri wangu wa hati ya kusafiria.

Hakimu: Kwa muda wote huo?

Mshtakiwa: Ndio.

Hakimu Ruboroga baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha kesi hadi April 16, 2024 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na kukosa wadhamini.