Mwandabila awataka wananchi wamuombee Rais Samia

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Songwe, Neema Mwandabila akiwa na baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Galula Kata ya Galula wilayani Songwe.

Songwe. Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Songwe, Neema Mwandabila amewataka wananchi wa Mkoa wa Songwe na Watanzania kumuombea Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ili azidi kuitenda kazi yake ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa urahisi.

Amesema kuwa kazi ya kuwahudumia wananchi ni ngumu hivyo inahitaji maombi ambayo yatamlinda na kumsaida kuzidi kuwa na hekima na busara katika uongozi wake.

Mbunge huyo ametoa rai hiyo wakati wa misa ya shukrani iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Galula liliyopo Kata ya Galula Wilayani Songwe huku akieleza kazi nzuri na mafanyiko ya Rais Samia hasa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

"Nitakuwa sijatenda haki kama sitaeleza mambo makubwa na mazuri anayoyafanya Rais amefanya mambo mengi kwa kipindi kifupi, kila mahali kuna miradi ya maendeleo inaendelea. Ujenzi wa shule, madarasa, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, maji, miundombinu, kila eneo miradi inatekelezwa," amesema na kuongeza.

"Kwa kuwa tupo kanisani niwaombe tumuombee Rais wetu ili aweze kuendelea kutuoongoza vizuri, anapambana kuwaletea maendeleo wananchi hivyo kazi yetu kubwa iwe kumshukuru kwa kumuombea," amesisitiza mbunge huyo.

Katika hatua nyingine mbunge huyo alichangia Sh300,000 za ukarabati wa kanisa hilo kongwe ikiwa ni kutimiza ahadi yake baada ya kushindwa kufika katika kipindi cha harambee iliyopita huku akiahidi kuwashonea zaidi ya watoto 20 sare katika kanisa hilo.

Pia, amewaahi wanakwaya wa Parokia hiyo kuwasaida kurekodi nyimba zaidi ya tatu kwa gharama zake katika studio bora watakayoitaka.

Amesema kuwa Mungu anampa riziki kila mtu kwa wakati wake hivyo yeye anafanya hivyo ikiwa ni majitoleo na sadaka yake kwa kumshukuru Mungu.

Mbunge huyo pia alitoa Sh500, 000 ambazo alikuwa anamalizia ahadi yake kwa kikundi cha akinamama wa Galula ambao walianzisha kikundi hicho kwaajili ya kuinuana kiuchumi.

Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Galula amemshukuru mbunge huyo kwa kufika kuisaidia parokia hiyo huku akibainisha kuwa watazidi kumuombea ili aweze kuendelea kuwatumika wananchi kwa amani.

Amesema kuwa mbunge huyo ameonyesha unyenyekevu kwa Mungu na kwa wananchi wa Galula kwa kuwa alishindwa kuhudhuria katika harambee ya ukarabati wa kanisa hilo lakini ametafuta nafasi ili aweze kufika katika kanisa hilo, hali ambayo baadhi wakipata nafasi za uongozi wanashindwa kuwa na karama ya unyenyekevu

Paroko huyo amesema kuwa Mwandabila ameonesha kuwa uongozi ni wito kwa kuonyesha unyenyekevu huo huku akizidi kumuomba kuendelea kuchangia ukarabati wa kanisa hilo ombi ambalo mbunge huyo alilipokea na kuwaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwaajili ya maboresho ya kanisa hilo kongwe ambalo ni moja ya makanisa kongwe nchini liliozinduliwa mwaka 1901.

Hata hivyo, baadhi ya wakinamama ambao wamepata msaada kutoka kwa mbunge huyo wamemshukuru huku wakimuahidi kuwa fedha alizozitoa zimewasaidia katika kuwainua kiuchumi hivyo wanathamini na kutambua mchango wake katika kuwasaidia wananchi.