Mabadiliko ya kishindo KKKT

Arusha. Ni mabadiliko ya kishindo. Hivi ndivyo unavyoweza kuelezea uamuzi wa wajumbe 214 kati ya 248 wa mkutano mkuu wa 21 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuridhia pendekezo la dayosisi zote kuwa na katiba moja.

Kwa mabadiliko hayo, katiba hiyo mpya inakwenda kuondoa zile za dayosisi 27 zinazotoa mamlaka kamili ya kujiendesha, badala yake KKKT inakwenda kuwa na mkuu wa kanisa mwenye mamlaka zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Kupitishwa kwa pendekezo hilo, kunamaanisha kuwa mkuu wa kanisa atakuwa na uwezo wa kuwachukulia hatua maaskofu na wachungaji wanaokiuka maadili.

Hata hivyo, mkuu wa kanisa hatafanya hivyo peke yake, bali kwa kutumia chombo cha kikatiba kitakachoundwa.

Muundo huu, unalenga kuwa tiba iliyotafutwa kwa muda mrefu ya namna ya kushughulikia migogoro na nidhamu katika dayosisi mbalimbali.

Kwa katiba iliyokuwepo, kila dayosisi ilikuwa mamlaka kamili na vyombo vyake vya maamuzi, jambo lililokuwa linaleta ugumu kwa mkuu wa kanisa kuingilia wakati wa mivutano.

Hata hivyo, chini ya mabadiliko hayo, inaelezwa kila dayosisi itaendelea kuwa na askofu wake, msaidizi wa askofu na vyombo vyake, ambavyo sasa vitaendeshwa kwa kutumia kanuni ndogo ndogo zitakazotungwa.

Akitangaza uamuzi huo jana mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Makumira (Tuma), Mkuu wa Kanisa hilo anayemaliza muda wake, Askofu Fredrick Shoo alisema asilimia 86 ya wajumbe wameridhia pendekezo hilo.

Askofu Shoo, ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, alisema idadi ya wapigakura ilipaswa kuwa 252, ila waliokuwepo ni 248 na kati yao, 214 walipiga kura za Ndiyo, sawa na asilimia 86 na za Hapana zilikuwa 36, sawa na asilimia 14.

"Hakuna kura iliyoharibika na hili nalifurahia sana, asanteni sana. Inaonyesha ukomavu wa wajumbe na kwa maana hiyo basi patano letu limepita kwamba KKKT tuwe na katiba moja kwa asilimia 86 ambazo ni zaidi ya theluthi mbili," alisema.

Vyanzo ndani ya mkutano huo, vilisema pendekezo hilo lilipowekwa, walipewa nafasi hiyo wajumbe sita au wanane, lakini hakuna askofu aliyepata nafasi, licha ya kuwepo walionyoosha kidole kutaka kuchangia.

“(Hao wajumbe) waliwaambia maaskofu wakae kimya ili wao ndio wazungumze kwa kuwa ndio wenye kanisa. Mmoja akataka hadi maaskofu watubu kwa kutomtii mkuu wa kanisa,” kilieleza chanzo hicho.

Chanzo hicho ambacho kiliomba jina lake lisitajwe, kilidokeza kuwa baadhi ya maaskofu walitaka kuhoji suala hilo kwa kuwa lilishawasilishwa katika kikao cha halmashauri kuu Aprili 2023 mkoani Shinyanga, lakini hawakufikia mwafaka.


Waunga mkono mabadiliko

Akizungumza baada ya uamuzi huo, Mwanasheria wa KKKT, Azaeli Mweteni alisema katiba moja iliyoridhiwa na wajumbe, itaondoa katiba za dayosisi.

"Kisheria ni kwamba mkutano mkuu wa 21 wa KKKT umepitisha mchakato wa katiba moja ya kanisa kwa sababu lililetwa pendekezo la kuandaa katiba moja ambayo itaziondoa nyingine za dayosisi na kuwa na moja,” alisema.

“Katika katiba hii ni kwamba imelenga kuliongezea nguvu kanisa ili liendelee kuwa moja kama ambavyo imekusudiwa," alisema mwanasheria huyo na kuongeza:-

"Hii italeta mabadiliko ya kiutendaji, lakini pia kuimarisha mfumo wa kiutawala, mfumo wa kiuongozi katika kanisa na kuendelea kuimarisha kanisa kuwa moja na kuimarisha uwajibikaji ndani ya kanisa," alifafanua.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo kutoka Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Aneth Mnzava alisema kanisa kuwa na katiba moja itasaidia kutekeleza dhana ya umoja na kanisa litakuwa na nguvu zaidi kuliko sasa kila dayosisi ina katiba yake.

"Kanisa ni uwakilishi wa Mungu hapa duniani, umoja wetu wa kanisa ndiyo ishara ya anachotaka Mungu, kuwa na katiba moja kunatekeleza kwa vitendo dhana ya umoja kwa sasa hivi tulivyo,” alisema.

“Kwa wale wanaofuatilia historia ya KKKT wanafahamu kwamba tulianza na makanisa saba, tukawa na dayosisi saba na kila dayosisi ilikuwa na nguvu yake, ila tunaona kule juu kunatakiwa kuwe na nguvu zaidi," alisema.

"Tunapokuwa na katiba moja itatupatia nafasi au fursa ya kusema KKKT kuanzia juu ni wamoja na katika dayosisi zetu ni watekelezaji wa moja kwa moja wa yale yanayotoka juu, ina maana kwamba mamlaka yetu itakuwa na nguvu zaidi.

“Itakuwa na sauti ya kusikika kutoka kwa mchungaji mmoja tunayemsikiliza, kwa hivyo nafikiri ni uamuzi mzuri uliofanyika," alifafanua Dk Aneth, kauli ambayo inaonekana kuungwa mkono na baadhi ya wajumbe wengi wanaounga mkono.

Hata hivyo, baadhi ya wajumbe walisema wanaamini mchakato huo wa mabadiliko utakuwa shirikishi hadi chini kwenye sharika na wanafikiri wazo hilo na rasimu vitashushwa chini vijadiliwe.

“Mimi sijaiona hiyo rasimu itafananaje, lakini nilifikiri hili pendekezo lingeanzia kule kwenye mitaa na sharika zetu halafu wakiridhia ndio lipande juu. Hili kidogo naona tofauti linaanzia juu kushuka chini. Naamini tutashirikishwa kikamilifu,” alisema mmoja wa wajumbe.

Katika hatua nyingine, kikao cha halmashauri kuu ya KKKT cha kupokea majina ya maaskofu watatu wanaopendekezwa na maaskofu wenzao kugombea nafasi ya mrithi wa Askofu Shoo kilianza saa 11:40 jioni jana.

Awali ratiba hiyo ilionyesha masuala yote ya uchaguzi yangefanyika kati ya saa 4:30 asubuhi hadi saa 6:30 mchana, lakini haikuwa hivyo.

Nje ya kikao hicho, taarifa zilizokuwa zikivuma awali zilidai huenda kukatolewa hoja kuwa Askofu Shoo aendelee kwa kipindi cha miaka miwili ili aweze kusimamia mchakato wa katiba moja itakayosimamia uendeshaji wa kanisa.

Hii iliongeza shauku ya wafuatiliaji wa mkutano huo wakitaka kufahamu kama hilo lingetokea na iwapo majina ya maaskofu wale wanne waliokuwa wanatajwa yangerudishwa na halmashauri kuu ili yapigiwe kura.

Mapema, majina ya maaskofu wanne yalikuwa yanatajwa kuwa na sifa za kumrithi Dk Shoo, ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mkuu wa kanisa hilo Agosti 2015, akimrithi Askofu Dk Alex Malasusa.

Majina yaliyokuwa yakitajwa kabla ya jana ni ya Dk Benson Bagonza (Karagwe), Dk Abednego Keshomshahara (Kaskazini Magharibi), Dk Msafiri Mbilu (Kaskazini Mashariki) na Dk Blaston Gavile (Iringa).