Wagombea wa KKKT kumrithi Askofu Shoo hawa hapa

Muktasari:

  • Mmoja kati ya hawa ndiye atakayemrithi Askofu Shoo, hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya majina ya wagombea wa nafasi ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kutangazwa rasmi usiku huu.

Arusha. Mmoja kati ya hawa ndiye atakayemrithi Askofu Shoo, hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya majina ya wagombea wa nafasi ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kutangazwa rasmi usiku huu.

Katika majina hayo, pia yumo aliyewahi kuwa Mkuu wa Kanisa hilo 2007-2015, Askofu Alex Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Majina hayo yametangazwa usiku huu, Agosti 24, 2023 na Askofu Shoo mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 21 wa KKKT, unaofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Tuma), ambapo zoezi la kupiga kura linaendelea ukumbini kwa sasa.

Wagombea wengine ambao wamependekezwa na maaskofu wenzao ni Askofu Abednego Keshomshahara wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, na Askofu George Mark Fihavango wa Dayosisi ya Kusini.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi katika mkutano huo ni Askofu Amon Mwenda wa Dayosisi ya Ruvuma, ambapo matokeo ya uchaguzi huo yatatangazwa baada ya kukamilika kwa kazi ya kuhesabu kura.