Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwendokasi kurejea Kibaha, furaha iliyogubikwa na 'kilio' kwa abiria

Muktasari:

  • Ruti ya usafiri wa mwendokasi Kibaha-Kimara hadi Mloganzila ilianza wakati wa utawala wa awamu ya tano wa hayati John Magufuli, kabla ya kusitishwa Septemba 2024.



Dar es Salaam. Wakati huduma ya mabasi ya mwendokasi ikirejesha safari za Kibaha- Kimara kuanzia Julai 6, 2026, ongezeko la nauli na safari kuishia Kimara kumeibua sintofahamu kwa abiria.

Usafiri huo wa umma kwenye njia ya Kibaha ulisitishwa tangu mwaka juzi kabla ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, jana Jumanne, Juni 30, 2026 kutangaza utarejea tena kuanzia Jumatatu ya Julai 6, 2026.

Ofisa Habari wa Halmashauri hiyo, Neto Kredo amesema safari hizo zitaanzia Stendi ya Kibaha na itaishia Kimara pekee.

Awali, kabla ya kusitishwa, njia ya Kibaha ilikuwa na safari pia ya Gerezani asubuhi na jioni ambayo kwa sasa haitakuwepo hadi itakapotangazwa hapo baadaye.

Hata hivyo, kiwango cha nauli na safari kuishia Kimara kumepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wakazi wa Kibaha.

Baadhi wameonyesha wasiwasi wa nauli kutoka Sh700 ya awali hadi Sh2,000 wakidai inaweza kuwa kikwazo kwa wengi wao kuutumia usafiri huo wa umma.

Wengine wamekwenda mbali zaidi na kuhoji kwa nini safari za Kibaha-Gerezani haijarudishwa wakionyesha wasiwasi wa kituo cha Kimara kitakavyopokea abiria wengi.

Wamesema pamoja na kuwa na furaha ya kurejeshwa kwa usafiri huo Kibaha, mambo hayo mawili yanaweza kusababisha usumbufu.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Julai Mosi, 2026, wengi wao wameeleza furaha ya kurejeshwa kwa usafiri huo wa umma licha ya kuonyesha wasiwasi wa ukubwa wa nauli na hofu ya usumbufu kupata usafiri mwingine wakifika Kimara.

"Nauli ya Sh2,000 ni kubwa mno, bora ingekuwa gharama hiyo ni kutoka Kibaha hadi Gerezani, lakini inaishia Kimara hapo tena uongeze 1,000 kwenda Gerezani au Kivukoni, bado haujarudi, achilia mbali ile panda shuka kusubiri usafiri mwingine Kimara," amesema Nailat Mbegu.

Mkazi mwingine, Felcian John amesema kupandisha bei karibu mara tatu kunaweza kuwa changamoto ya wengi kushindwa kuimudu na kuendelea kutumia daladala.

"Mfano nikiwa natoka kwa Mathias, nikipanda daladala hadi Mbezi ni 1,500, kisha Mbezi nikitumia mwendokasi ni Sh1,500 hivyo nakuwa nimetumia Sh3,000.

"Lakini nikisema nikapande mwendokasi Kibaha, kwanza lazima nipande daladala Sh700 kutoka kwa Mathias hadi Stendi ya Kibaha ili nikapande mwendokasi Sh2,000, nikifika Kimara nipande tena jingine Sh1,000 hapo sina uhakika wa siti," amesema.

Amesema kama mamlaka zingeweka bei hiyo ya Sh2,000 au hata Sh2,500 hadi Gerezani ingekuwa nafuu kwa wenye kipato cha chini na usafiri huo wa umma ungewasaidia wengi.

Kwa Agripina John yeye amekuwa tofauti akibainisha kwamba nauli sio kikwazo sana, tatizo ni ruti ya kuishia Kimara akishauri ingekuwa rahisi kwa wananchi kama ruti ya moja kwa moja Kibaha-Gerezani au Kivukoni ingekuwepo kwa gharama au zaidi hata kufika Sh3,000.

"Hata nauli ingekuwa Sh3,000 ingekuwa sawa, lakini ruti iwe ya moja kwa moja kutoka Kibaha kwenda Gerezani au Kivukoni, tofauti na hii panda shuka tukifika Kimara kuanza kuhangaika tena kugombea usafiri pale," amesema.

Amesema Kimara yenyewe ina watu wengi wanaotegemea usafiri huo, achilia mbali wale wanaotoka Mloganzila na kushushwa pale na wale wa Mbezi pia wanashushwa pale na kusubiri mabasi kwenda maeneo mengine ya Dar es Salaam.

"Hapo na sisi wa Kibaha tunakwenda kumwaga (kushushwa) pale, hiyo ‘nyomi’ itakuwaje Kimara? Bora ingekuwa ukipanda basi Kibaha basi ni moja kwa moja hadi Gerezani au Kivukoni lakini kwa Kimara hofu yangu ni watu watakuwa wengi kwenye hicho kituo na tutarudi kulekule kugombania kuingia kwenye mabasi hadi kuumizana,." amesema.

Kuhusu kuwepo kwa ruti ya moja kwa moja Kibaha Gerezani, Kredo amesema bosi wake ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha anaendelea kupokea maoni na changamoto zote kutoka kwa wananchi wakati ruti ya Kimara ikiwa inaendelea hivyo itafanyiwa kazi.

"Mkurugenzi wetu katika mkakati wa kurejesha ruti hii, aliona kwanza ianze hii ya Kibaha- Kimara, ikiwa inaendelea basi na hizi changamoto zingine ndogondogo zitaendelea kutatuliwa," amesema.

Amesema katika ruti hiyo inayoanza Jumatatu ijayo usafiri huo utatoa huduma kuanzia saa 12:00 asubuhi na utakuwepo muda wote.