Mwenge wa Uhuru kupokewa Kilimanjaro Juni 6
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai
Muktasari:
Wakati Mwenge wa Uhuru ukitarajiwa kupokewa Mkoani Kilimanjaro Juni 6 mwaka huu Mkuu wa Mkoa huo,Stephen Kagaigai amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea huku akiwahakikishia usalama wa kutosha.
Moshi. Wakati Mwenge wa Uhuru ukitarajiwa kupokelewa mkoani Kilimanjaro Juni 6 mwaka huu Mkuu wa Mkoa huo,Stephen Kagaigai amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea mwenge huo huku akiwahakikishia usalama wa kutosha.
Kagaigai ameyasema hayo leo Juni Mosi 2022 wakati akitoa taarifa ya ujio wa mwenge huo, mkoani humo kupitia Wilaya ya Same ukitokea Tanga.
"Tunatarajia kupokea Mwenge wa uhuru kutokea mkoani Tanga Juni 6 mwaka huu katika kijiji cha Bendera Wilaya ya Same utakimbizwa katika Halmashauri zote 7 za mkoa huu, kuanzia Juni 6 hadi Juni 12.
"Wakati tukiupokea Mwenge wa uhuru mkoani kwetu niwahakikishie wananchi wote suala la usalama litazingatiwa kwa kiwango cha hali ya juu kama ilivyo kawaida kwa mkoa huu,hivyo wananchi wasiwe na hofu juu ya usalama wao wakati wote wa ujio wa mwenge na wakati utakapopita katika maeneo yenu,"amesema Kagaigai
Amesema, Mwenge wa uhuru utakapokuwa mkoani humo utatembelea miradi mbalimbali, kukagua na kuweka mawe ya msingi kwa miradi inatekelezwa kupitia fedha za Serikali.
Amesema miradi ambayo itapitiwa na mwenge wa uhuru ni miradi ya elimu,afya,maji,miundo mbinu ya barabara ikiwamo iliyofadhiliwa na fedha zinazotolewa za uviko 19, tozo za simu pamoja na miradi inayotekelezwa na vikundi mbalimbali vya vijana na wanawake na watu wenye ulemavu ambazo ni fedha zinazotokana na mikopo ya Halmashauri.
Kagaigai amesema ujumbe wa Mwenge wa uhuru mwaka huu umebeba kauli mbiu ya sensa ya watu na makazi usemao "Sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo shiriki kuhesabiwa tuyafikie maendeleo ya Taifa,"