Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwenge wazindua madarasa shule iliyoezuliwa na upepo, mvua 2022

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Godfrey Mzava akizungumza jambo na viongozi wa Wilaya ya Momba baada ya kuzindua vyumba viwili vya madarasa shule ya msingi Ntungwa. Picha na Denis Sinkonde

Momba. Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Mzava leo Septemba Mosi, 2024, amezindua vyumba viwili vya madarasa vilivyojengwa katika Shule ya Msingi Ntungwa, iliyopo Kata ya Mkomba, wilayani Momba, mkoani Songwe.

Uzinduzi huo umeondoa changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo.

Shule ya Msingi Ntungwa, ilikumbwa na uhaba wa vyumba vya madarasa baada ya mapaa ya vyumba viwili kuezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali mwaka 2022.

Hali hiyo iliifanya ibakiwe na vyumba vitatu pekee kati ya saba vilivyokuwepo awali.

Akisoma risala ya ujenzi wa mradi huo mbele ya kiongozi wa Mwenge, Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Momba, Maiko Nzunda amesema mradi huo umegharimu Sh45.7 milioni.

“Fedha hizi zimetumika kujenga vyumba viwili vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu. Tumeukamilisha mradi huu ambao umetusaidia kupunguza kidogo adha ya mrundikano wa wanafunzi darasani,” amesema mwalimu huyo.

Amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 498, wakiwemo wasichana 269 huku akisema bado inahitaji vyumba 13 vya madarasa, vilivyopo ni vitano pekee.

Hivyo, amesema kukamilika kwa vyumba hivyo vipya kutasaidia kidogo kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

"Awali shule hii ilikuwa na vyumba saba vya madarasa, lakini mwaka 2022 upepo mkali ulioambatana na mvua uliezua paa la shule na kubakiza vyumba vitatu pekee. Baada ya Serikali kutoa fedha na kujenga vyumba hivyo, shule sasa ina vyumba vitano, lakini bado tunahitaji saba zaidi," amesema Nzunda.

Mariam Mbuzi, mmoja wa wanafunzi shuleni hapo amesema ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia.

“Lakini pia tulikuwa tunarundikana darasani, walau tutapumua kidogo lakini hali bado. Ila sasa tutasoma vizuri,” amesema mwanafunzi huyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ntungwa, Justine Mgode ameishukuru  Serikali kwa kujenga vyumba hivyo, lakini ameiomba iongeze fedha zingine kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vingine kwa kuwa bado kuna uhaba.

Akizungumza baada ya kuzindua vyumba hivyo vya madarasa, Mzava amesema ameridhishwa na ujenzi wake kwa kuwa wamezingatia taratibu za manunuzi.

"Hakikisheni mnatunza miundombinu ya majengo ili idumu kwa muda mrefu na itumike kwa vizazi na vizazi kwa ajili ya kupata elimu," amesema Mzava.