Mwenyekiti CCM Kibaha ashindwa kutetea…

Mwenyekiti mpya wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini Mkoa wa Pwani Mwajuma Nyamka. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini mkoani Pwani, Maulidi Bundala ameshindwa kutetea nafasi yake baada ya Mwajuma Nyamka kuibuka na ushindi wa nafasi hiyo.

Kibaha. Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini mkoani Pwani, Maulidi Bundala ameshindwa kutetea nafasi yake baada ya Mwajuma Nyamka kuibuka na ushindi wa nafasi hiyo.

Nyamka alitangazwa mshindi wa nafasi hiyo baada ya kupata kura 346 huku Bundala akiambulia kura 173 kwenye uchaguzi wa nafasi hiyo uliofanyika Jumapili Oktoba 2, 2022 Mjini Kibaha.

Wagombea wengine katika nafasi hiyo ni Sauda Mpambalioto aliyepata kura 33 na Abdalah Mdimu akipata kura 32.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi kwenye nafasi hiyo Nyamka amesema kuwa baada ya uchaguzi huo kukamilika kinachofuatia ni kufanya kazi na si kuendeleza makundi.

"Naomba niseme kwa kuwa nitakuwa mkali kwa viongozi watakaoonekana kuingilia majukumu yasiyowahusu kwani kufanya hivyo ni kuvuruga utaratibu wa uwajibikaji" amesema.

"Hapo nitakuwa mkali kwa wale watakaojiita mwenyekiti ajaye au diwani ajaye huo siyo utaratibu wa chama chetu tunapaswa tufanye kazi kwa upendo ushirikiano na kudumisha amani iliyopo" amesema.

Kwa upande wake Bundala amesema kuwa ingawa ameshindwa kutetea nafasi yake lakini bado ataendelea kuta ushirikiano kwa kiongozi aliyeshinda ili kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushika dola.

Mbapambalioti amesema kuwa kura alizopata ndiyo halali yake lakini alizaliwa kwenye CCM na atakuwa humo hadi mwisho wa maisha yake.

Naye Abdalah Mdimu amesema kuwa kushindwa kupata nafasi ya uenyekiti hakuwezi kumkatisha tamaa ya kuendelea kuitumikia chama hicho bali yuko tayari kutoa ushirikiano kwa hatua zozote pindi anapohitajika.