Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwili wa Akwilina kuagwa leo, familia yatoa mchanganuo gharama za Serikali

Waombolezaji wakiwa msibani nyumbani kwa Tegolena Uiso, ambaye ni Dada wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), marehemu Akwilina Akwiline aliyeuawa kwa kupigwa risasi. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Akwilina aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), mwili wake unaagwa katika viwanja vya chuo hicho, huku familia ikitoa mchanganuo wa namna Serikali itakavyogharimia mazishi yake.

Dar es Salaam. Saa zaidi ya 120 tangu alipopigwa risasi Akwilina Akwiline na kusababisha simanzi na mijadala mbalimbali nchini, sasa binti huyo ataagwa jijini Dar es Salaam leo.

Akwilina aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), mwili wake unaagwa katika viwanja vya chuo hicho, huku familia ikitoa mchanganuo wa namna Serikali itakavyogharimia mazishi yake.

Kifo cha Akwilina kilitokana na kupigwa risasi na polisi Februari 16 akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana kwenda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao walioshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni, Februari 17.

Familia ya marehemu juzi ilitoa bajeti ya mazishi ya Akwilina ikisema yatagharimu Sh80 milioni.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika taarifa iliyotolewa jana kupitia kwa katibu mkuu wake, Dk Leonard Akwilapo ilikiri kupokea bajeti hiyo ya Sh80 milioni kutoka kwa msemaji wa familia, Festo Kavishe.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha wizara hiyo, Mwasu Sware alisema baada ya kupokea makisio hayo, Dk Akwilapo alitahadharisha kuwa kuna baadhi ya matumizi hayatakubaliwa kwa kuwa kisheria hayagharimiwi na Serikali. Pia, alisema katika makisio hayo kuna gharama ambazo zipo juu.

Alisema katibu mkuu aliagiza kuwe na kikao kati ya wizara na ndugu wa marehemu ili kuweka sawa changamoto hizo ili kuwa na bajeti ya pamoja. Kikao hicho kilifanyika juzi na kufikiwa muafaka.

Kutokana na hilo, katibu wa kamati ya mazishi Moi Kiyeyeu ambaye ni kaka wa Akwilina alisema jana kuwa Serikali haitawapatia fedha taslimu bali itanunua jeneza, nguo za marehemu, maua na mashada.

Itatoa magari matatu, kati ya hayo moja litabeba mwili wa marehemu na watu wanne na magari mawili aina ya Toyota Coaster yatabeba waombolezaji wanaokadiriwa kufikia 60 watakaokwenda wilayani Rombo, Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika kesho.

Kiyeyeu alisema Serikali itagharimia utengenezaji wa kaburi, manukato, chakula, maturubai, viti na muziki ambavyo vyote viliorodheshwa kwenye bajeti ya familia.

Alisema Serikali imekuwa ikipeleka chakula nyumbani kwa dada wa marehemu Akwilina, Mbezi Louis na kwamba itashughulikia mazishi chini ya uratibu wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rombo.

“Serikali imetutaka kutoa stakabadhi kwa vitu ambavyo tulivifanya awali ili kuangalia namna ya kurejeshewa fedha,” alisema.

Kiyeyeu alisema walitarajia kusafiri na watu takriban 200, sasa wanajipanga kuona jinsi wengine watakavyosafiri.

Kuhusu gharama za chakula njiani, Kiyeyeu alisema Serikali itagharamia kwa ambao watakuwa kwenye magari hayo matatu.

“Tulipotoa bajeti (Sh80 milioni) hatukuwa na maana ya kuishinikiza Serikali itoe fedha zote bali ilikuwa mahitaji ya msiba hadi pale utakapoisha. Tunashukuru Mungu kwa Serikali kuridhia kugharimia,” alisema.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Elimu, mwili wa Akwilina utawasili viwanja vya NIT saa sita mchana na kutafanyika ibada mpaka saa saba mchana.

Kutasomwa historia ya marehemu na kufuatiwa na salamu za rambirambi kisha neno la shukrani na baadaye kuaga mwili wa Akwilina. Safari ya Rombo inatarajiwa kuanza saa tisa alasiri.

Kifo cha Akwilina

Baada ya kusambaa taarifa za Akwilina kupigwa risasi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa Februari 17 alikiri kuwapo kwa kifo cha mtu mmoja aliyepigwa risasi na askari wakati wakizuia maandamano ya Chadema.

Kutokana na tukio hilo, Mwananchi Februari 17 lilizungumza na dereva na kondakta wa gari alilokuwa amepanda Akwilina walioeleza mkasa mzima ulivyotokea.

Februari 18, viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Rais John Magufuli walitoa pole kwa familia ya Akwilina, baadhi kupitia mikutano na waandishi wa habari na wengine kwenye mitandao ya kijamii.

Ni siku hiyohiyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alitangaza kushikiliwa askari sita kwa uchunguzi pamoja na silaha zao.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akiambana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni walitangaza Serikali kugharimia mazishi hayo.