Mwili wa bosi wa Chako ni Chako kuzikwa Alhamisi
Muktasari:
- Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Baa maarufu jijini Dodoma Chako ni Chako, Honorath Makoi aliyefariki dunia kwa ajali ya gari usiku wa kuamkia jana unatarajiwa kuzikwa nyumbani kwao Kibosho mkoani Kilimanjaro siku ya Alhamisi.
Dodoma. Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa baa maarufu jijini Dodoma ya ‘Chako ni Chako’, Honorath Makoi unatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Kibosho, mkoani Kilimanjaro Alhamisi ya Novemba 7, 2024.
Makoi (35) amefariki dunia alfajiri ya saa 10 jana Jumapili Dodoma kwa ajali baada ya gari alilokuwa akiendesha kuacha njia na kugonga mti wakati akirejea nyumbani kwake Swaswa jijini humo.
Maiko amefikwa na mauti akiwa ameshamvisha pete mchumba wake na kilichokuwa kikisubiriwa na kufunga ndoa.
Akizungumza leo Jumatatu Novemba 4, 2024 na Mwananchi, msemaji wa familia ya marehemu, Hendry Sindato amesema mipango ya mazishi ya Makao inafanyika nyumbani kwake Swaswa na mwili wake unatarajiwa kuagwa Jumatano ya wiki hii na kisha kusafirishwa kwenda Kibosho kwa maziko.
“Marehemu alikuwa bado hajaoa, ila alikuwa na mchumba ambaye sisi kama familia tulikuwa tunamtambua kwa sababu tayari alishamvisha pete, ilikuwa bado tu kuoana na walikuwa hawajapata mtoto …ila kama alikuwa na watoto huko nje tutajua baadaye,” amesema Sindato.
Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa baa hiyo, Amani Moshi amesema baa hiyo itafungwa mpaka mkurugenzi huyo atakapozikwa Alhamisi na huduma zitarejea kuanzia Ijumaa baada ya maziko.
Amesema mkurugenzi huyo alipata ajali wakati akitoka kwenye baa yake mpya aliyoifungua hivi karibuni inayoitwa Ze Evick, alipokuwa akirudi nyumbani ndipo alipopata ajali hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi uliosababisha dereva kushindwa kuthibiti gari na kutoka kwenye barabara na kugonga mti uliokuwa njiani.
Pia, Kamanda Katabazi ametoa taarifa ya ajali nyingine iliyotokea jana usiku eneo la Dodoma Makulu njia ya kwenda Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambapo Erick Sichila (37) aliyekuwa akiendesha gari huku amelewa alishindwa kulithibiti gari lake na kugonga bajaji mbili, pikipiki mbili na gari moja.
Amesema katika ajali hiyo hakuna aliyepoteza maisha, isipokuwa uharibifu wa vyombo vya moto na kusababisha majeruhi watatu, akiwemo dereva huyo anayetibiwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi.