Mwili wa Gardner wapelekwa nyumbani kwake Kijitonyama

Jeneza lenye mwili wa Gardner Habash likipokea nyumbani kwake Kijitonyama leo Aprili 21, 2024. 

Muktasari:

  • Mawaziri Nape, Ummy waeleza umahiri wa Gardner, watoa neno kwa waandishi wa habari wanaochipukia

Dar es Salaam. Mwili wa Gardner Habash umepelekwa nyumbani kwake Kijitonyama na kesho Aprili 22, 2024 utaagwa katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam.

Gardner aliyekuwa mtangazaji wa kipindi cha Jahazi kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds FM, alifariki dunia alfajiri ya Aprili 20, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mwili ulifikishwa nyumbani hapo saa 12.00 jioni na kupokewa na waombolezaji wakiwamo wafanyakazi wa Clouds Media Group alikokuwa akifanya kazi kama mtangazaji.

Waombolezaji wamekuwa wakifika kutoa pole kwa ndugu na jamaa, akiwamo Careen maarufu 'Malkia Careen ambaye ni mtoto wa Gardner.

Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said aliyekuwa miongoni mwa waombolezaji amesema amepoteza si tu shabiki bali mwanachama wa klabu hiyo.

"Ninachokikumbuka na siwezi kukisahau na nilimwambia mwenyewe ni namna alivyokuwa anatangaza, nilitamani siku moja nimwambie na nilipofanya mahojiano nilimwambia," amesema Hersi.

Amesema walikuwa wakizungumza mambo mengi si ushabiki wa Yanga pekee, bali pia kushabikia timu ya Uingereza ya Liverpool.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Gardner alikuwa na uwezo wa kuangalia jambo ambalo ni habari na kuitafsiri kwa lugha rahisi na ujumbe ukafika.

“Mara nyingi wakati tunajifunza uandishi wa habari wakati mwingine tunaweka ugumu wa habari, yeye anaweza kukuta habari ngumu akarahisisha ikawa rahisi na kutafsirika vizuri, kuieleza kwa lugha ya kawaida na unakuta jambo ni kubwa,” amesema.

Nape amesema alikuwa akipokea jambo hulichambua kisha kulipeleka kwa hadhira ambayo ilikuwa inamsikiliza kwa lugha na sauti nzuri ambayo ilikuwa inavutia kusikilizwa.

Amesema ilikuwa ni ngumu kupita kutafuta stesheni ya kusikiliza.

Nape ameshauri watangazaji vijana kuiga sanaa na uwezo wa kutafsiri kwa mazingira halisi ambayo yaweza kuwapa mashabiki na wapenzi wengi kwa tumia lugha yao.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema atamkumbuka Gardner wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 mwaka 2020 alikuwa anatumia kipindi cha Jahazi kutoa taarifa na ufafanuzi.

“Kilikuwa kipindi kizuri binafsi nilikuwa siwezi kukataa mwaliko wa kuongea katika kipindi cha Jahazi kwa sababu ya Gardner na washirika wenzake,” amesema.

Amewataka wanahabari wanaochipukia kujifunza utendaji kazi kutoka kwa Gardner na kuamini kuwa Clouds Media wataandaa  andiko ambalo litawasaidia wanahabari wachanga jinsi ya kufanya utangazaji wenye mvuto na ushawishi kwa jamii.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amesema kuna mambo mengi Gardner amefanya hususani kwenye kuhabarisha, kuhamasisha na kuelimisha.

“Ni vigumu kupokea msiba lakini tumeumbwa na kifo tumekuja na tutapita hapa duniani mwenzetu ametangulia kazi yetu kubwa ni kumshukuru Mungu na kumuombea ili pale alipokosea Mungu aweze kumsamehe na kupumzika kwa amani,” amesema Mtambule.