Rais Samia aombolezo kifo cha Gardner wa Clouds Media

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameungana na waombolezaji wengine kutoa salamu za pole kutokana na kifo cha mtangazaji, Gardner Habash.

Gardner, aliyekuwa mfanyakazi wa Clouds Media Group (CMG) alifikwa na mauti jana Jumamosi, Aprili 20, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya shinikizo la damu.

Mwili wake utazikwa Jumanne ya Aprili 23, 2024 katika Kijiji cha Kikelewa, Kata ya Tarakea, Rombo mkoani Kilimanjaro.

Leo Jumapili, Aprili 21, 2024, Rais Samia ametumia akaunti zake za kijamii kutoa salamu za pole. Katika salamu hizo, mkuu huyo wa nchi ameweka picha ya Gardner akisema:

"Ninatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wafanyakazi wa Clouds Media Group kwa kuondokewa na ndugu yetu, Gardner Gabriel Habash."

Mchango wa Gardner kwenye ustawi wa sekta ya habari nchini ni mkubwa, na amekuwa mnasihi wa vijana wengi. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema. Amina."