Mwili wa Hayati Mwinyi kupita maeneo haya leo

Muktasari:

  • Mwili wa Rais Mwinyi utaagwa leo Ijumaa, Machi mosi, 2024 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ametaja maeneo ambayo mwili wa Hayati Rais Ali Hassan Mwinyi utapita kwa ajili ya kwenda Uwanja wa Uhuru kuagwa.

"Tumejipanga kwa msiba huu, njia ambazo zitatumika zitakuwa mbili, njia ya kwanza ni kutoka Mikocheni tutapita Shoppers pale Morocco lakini tutakwenda msikitini kwa ajili ya ibada,” amesema Kamanda Muliro.

“Tukitoka kwenye ibada tutarudi kutoka Morocco kwenda Magomeni kwa maana tutapita Manyanya, Mkwajuni hadi Kigogo na tutapita karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Baada ya ofisi hiyo takwenda hadi Veta mpaka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce) na kuishia Uwanja wa Uhuru, hizo ndio njia tutakazotumia, kwa hiyo wananchi watakaopenda kuwa barabarani watakuwa kwenye njia hizo.”

“Polisi na vyombo vingine vya dola tumejipanga kwenye maeneo hayo, utaratibu mzuri utakuwepo pale uwanjani ndani na nje, watu wanahimizwa waje kumuaga mpendwa wetu,” amesema Kamanda Muliro.

Mwili wa Rais Mwinyi utaagwa leo Ijumaa, Machi mosi, 2024 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mzee Mwinyi alifikwa na mauti saa 11.30 jioni ya jana Alhamisi, Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu.

Rais Samia Suluhu Hassan ndiye alitangaza kifo chake na kutangaza siku saba za maombolezo kuanzia leo Ijumaa na bendera zikipepea nusu mlingoti.


Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi.