Mzee Ruksa: Maisha na siasa za Tanzania

Muktasari:

  • Maisha ya Ali Hassan Mwinyi aliyezaliwa Mei 8, 1925, yamehitimishwa baada ya kifo chake kilichotokea jana Februari 29, 2024.

Dar es Salaam. Huyu ni Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1985-1995), ambaye pia amewahi kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (Januari 30, 1984 – Oktoba 24, 1985) nafasi iliyomfanya awe pia Makamu wa kwanza wa Rais.

Kabla ya hapo aliwahi kuwa Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) na baadaye Mambo ya Ndani ya nchi, Afya, Maliasili na Utalii, Ofisi ya Rais (Muungano) na Balozi nchini Misri.

Mzee Mwinyi akiwa Rais pia alikuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanzia 1990 hadi 1996 alipokabidhi kijiti kwa Benjamin Mkapa.

Mbali na nyadhifa hizo za uongozi, sehemu kubwa ya maisha yake anaisimulia mwenyewe katika kitabu chake cha ‘Mzee Ruksa; Safari ya Maisha yangu’.

Kwa mujibu wa kitabu hicho, Mzee Mwinyi alizaliwa katika Kijiji cha Kivule pembezoni mwa barabara kuu itokayo Dar es Salaam hadi Kisiju Pwani, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Alipotimiza umri wa miaka minne, baba yake alimpeleka Unguja kuanza masomo. Kituo chao cha kwanza kilikuwa kijiji cha wavuvi Mangapwani, kiasi cha kilomita 24 kaskazini magharibi mwa Unguja, akiishi nyumbani kwa rafiki wa baba yake aliyeitwa Mzee Suwedi bin Mgeni. Baada ya kupata elimu ya Qur'an kule Mangapwani chuoni kwa Maalim Khamisi wa Jirini, alihitimu kwa miezi minne tu baada ya kumudu kujua kusoma kwa muda mfupi kwa sababu, kwanza, alikuwa hakubali kushindwa na pili, alipenda sana kuimba kwa sauti kubwa kama ilivyokuwa tabia ya watu wa Mangapwani wa zama hizo.

Hii ilimsaidia kwa sababu badala ya kuimba nyimbo za kawaida zilizoimbwa na wengine, kama vile taarab, yeye alisoma (kuimba) sura za Qur'an na mtindo huo ulimsaidia sana.

Mwaka 1933 alianza kusoma katika Shule ya Msingi Mangapwani. Alhamisi ya Januari 5, 1933 alijikuta yumo katika darasa la kwanza la shule hiyo baada ya kufikishwa hapo na mlezi wake, Mzee Suwedi bin Mgeni.

Mwaka 1936 aliingia darasa la nne ambalo ndilo lilikuwa la mwisho katika Shule ya Mangapwani. Enzi hizo kulikuwa na shule mbili tu za Serikali zenye darasa la tano. Moja ilikuwa Zanzibar mjini na ya pili ilikuwepo Dole kijijini, Unguja.

Mwaka 1937 alijiunga rasmi na Shule ya Kati Dole, iliyokuwa ya bweni. Lengo la awali la shule hii lilikuwa kupokea wanafunzi kutoka shule za msingi za vijijini tu na mtaala wake ulikuwa uleule wa kumfikisha mwanafunzi mpaka kidato cha nne.

Kwa wakati wake, hapo shuleni walikuwapo wanafunzi 80. Mkuu wa Shule alikuwa Mwingereza; na walimu wote walikuwa Waarabu.

Katika kitabu chake hicho, Mwinyi anaeleza kwamba akiwa shuleni hapo ndipo alipoonja adha ya ubaguzi.


Ubaguzi wa rangi

Katika simulizi hiyo, Mzee Mwinyi anasema shuleni hapo kulikuwa na mabweni matano, kila moja likiwa na wanafunzi 16, kati ya hayo, anasema bweni namba moja lilikuwa la vijana wa Kiarabu peke yao, na mabweni yaliyofuata yakawa ya mchanganyiko.

Bweni namba tatu alilokuwamo yeye alijikuta wapo Waafrika weusi peke yao. Ubora wa huduma kwenye mabweni yao nao ukawa unapungua kuanzia bweni namba moja hadi tano.

Mathalani, anasema wenzao walipewa vitanda vya chuma, magodoro mazuri na vyandarua; lakini yeye na wenzake kwenye bweni namba tatu walipewa vitanda vya mbao vilivyo tandwa kamba (maarufu kama 'teremka tukaze'). “Magodoro yetu yalikuwa ya usumba”.

Siku moja, usiku wa manane, anasimulia, "bweni letu likavamiwa na kunguni wengi, idadi ambayo sikuwahi kuiona na wala sijaiona tena. Walikuwepo kunguni kila mahali mpaka sakafuni; ikawa hakulaliki tena."

Miongoni mwao wakajitokeza mashujaa wakasema hatukubali. Wakafunga safari kwenda kutoa taarifa kwa naibu mkuu wa shule; na alipofika kushuhudia aliwahurumia, akawaomba wavumilie wakati jambo hilo likishughulikiwa.

Anasimulia siku iliyofuata walikwenda kuweka dawa ya kuua kunguni, kisha wakaletewa vitanda vya chuma, magodoro na vyandarua kama wenzao wa mabweni mengine. Wakagundua kuwa tatizo halikuwa uwezo wa kuwapatia huduma sawa na wenzao wa mabweni mengine, bali ilikuwa ubaguzi tu.

Alimaliza darasa la tisa mwaka 1941. Baadaye, mwaka 1942, aliamua kujisomea mwenyewe darasa la kumi kupitia Rapid Results College ya Uingereza kwa njia ya posta. Mwaka 1943 na 1944 alisoma Chuo cha Ualimu Dole. Baada ya kumaliza mafunzo ya ualimu, alifundisha kijijini kwao Mangapwani mwaka 1945 na 1946. Mwaka 1947 alihamishiwa Bumbwini kuanzisha shule mpya.


Aenda kusoma ng'ambo

Aprili 1954 Mwinyi alipata barua kuwa Serikali imempa fursa ya kwenda kusomea ualimu nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Durham, karibu na Newcastle.

Baada ya kumaliza masomo alipewa hiari ya kuchagua aina ya usafiri kurejea kwao kati ya ndege au meli. Yeye na wenzake waliamua kutalii. Wakachagua kusafiri kwa meli. Mwaka 1961 alipelekwa tena na Serikali kwenye Chuo Kikuu cha Hull, Leicester, nchini Uingereza kujifunza mbinu za kufundisha ualimu kwa wanafunzi wa ualimu. Alikaa huko hadi aliporejea Zanzibar mwaka 1962 na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Ualimu.


Mapinduzi na Muungano

Miaka miwili baadaye, mwaka 1964, ndipo yakatokea Mapinduzi yaliyoung'oa utawala wa Sultan. Ingawa Mwinyi hakuwa mwasisi wa chama cha Afro Shiraz (ASP) wala hakushiriki moja kwa moja kwenye Mapinduzi, alikuwa mkereketwa, ikizingatiwa kuwa alikuwa mtumishi wa Serikali iliyokuwa madarakani kabla ya Mapinduzi.

Nafasi yake ya kwanza na ya siri kwenye siasa ilikuwa ya Katibu wa ASP wa Tawi la Makadara, Zanzibar mjini. Kwa upande wa mkewe, Mama Siti, walikuwapo wahusika wakubwa zaidi kwenye ASP, mmoja wao akiwa kaka yake ambaye alihusika kwenye Mapinduzi.

Siku chache baada ya mapinduzi hayo, Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwaka 1970, katika uchaguzi mkuu upande wa Tanzania bara uliofuatiwa na kuundwa kwa Baraza la Mawaziri. Ingawaje wakati ule vyama tawala ndani ya muungano (Tanu na ASP) vilikuwa havijaungana, Mwalimu Nyerere alijitahidi kuteua mawaziri kutoka Zanzibar, hata kwenye wizara ambazo hazikuwa za Muungano.


Alala mwalimu aamka waziri

Ndipo Desemba 1970 Mwinyi alipata ujumbe kuwa anaitwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Abeid Amani Karume. Alifuatwa na gari la Polisi, lakini alikataa kulipanda, akiwaambia waliomfuata yeye si mfungwa, kwa hiyo haoni kwa nini abebwe na gari la Polisi.

Badala yake akaenda kwa kuendesha gari lake mwenyewe aina ya Morris Minor hadi Ikulu, huku akifuatwa nyuma na gari la Polisi.

Baada ya kufika Ikulu, Rais Karume alimwambia Mwinyi: “Julius (Nyerere) kanipigia simu. Leo anateua Baraza la Mawaziri na angependa nipendekeze kijana mmoja anayefaa, mwenye elimu nzuri, amteue kuwa waziri. Anahitaji mtu mmoja lakini amenitaka nimpelekee majina mawili ili yeye mwenyewe achague moja.”

Mwinyi akabaki ameduwaa. Karume akaendelea kuongea, "Nimeamua nimpelekee hayo majina mawili, moja likiwa lako, ili awe huru kuchagua mmoja. Sikiliza taarifa ya habari ya saa mbili usiku leo. Utajua alivyoamua. Basi nenda!”

Mwinyi aliondoka kimyakimya kiasi kwamba alisahau hata kusema 'Ahsante, Mzee!' Alipofika nyumbani hakubanduka karibu na redio akingojea taarifa ya saa mbili usiku. Wakati taarifa inasomwa, akasikia ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais).

Kwake hii ilikuwa ni bahati njema. Alilala akiwa mwalimu, akaamka akiwa waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakukuwa na kugombea wala kuomba kura.

Siku iliyofuata alipelekewa ndege ya Serikali iliyompeleka Dar es Salaam kuapishwa pamoja na mawaziri wenzake. Hiyo ikawa ni mara yake ya kwanza kukutana ana kwa ana na Mwalimu Nyerere.

Hakupewa maelekezo yoyote kuhusu majukumu yake kwa nafasi aliyopewa. Akamuuliza aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dickson Nkembo, naye hakumpa jibu la moja kwa moja. “Basi kwa mwaka wote wa 1971 nikawa waziri lakini asiye na shughuli iliyotamkwa,” anasimulia.

Mwaka 1972, Mwalimu Nyerere alifanya mabadiliko mengine kwenye Baraza la Mawaziri na Mwinyi aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya. Aliendelea kushika wadhifa huo hadi ulipofanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 1975.

Ingawa hakugombea Katika uchaguzi huo, Mwalimu Nyerere alimteua kuwa mbunge na kisha akamteua kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.


Uwaziri mchungu

Akiwa  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (1975-1977) kilikuwa kipindi kichungu sana kwake. Ni wakati ambao yalitokea mauaji, mengine ya kutisha ya vikongwe kwenye mikoa ya Mwanza na Shinyanga yaliyosababishwa na imani za kishirikina. Wakati huo Waziri Mkuu alikuwa Rashidi Kawawa.

Jumamosi ya Januari 24, 1976 Kawawa aliitisha kikao kujadili kadhia hiyo na kutafuta njia ya kukomesha mauaji hayo. Kutokana na wadhifa wake wa uwaziri wa Mambo ya Ndani, Mwinyi alihudhuria kikao hicho.

Mwingine ambaye naye alikuwapo ni aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (mwenye dhamana ya Idara ya Usalama wa Taifa), Peter Siyovelwa; Wakuu wa Mikoa ya Mwanza (Peter Kisumo) na Shinyanga (Marco Mabawa), pamoja na maofisa wa juu wa Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa; na wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama wa mikoa hiyo.

Iliamuliwa kuanzishwe operesheni maalumu iliyoitwa 'Operesheni Mauaji’ kwa lengo la kuwakamata na kuwahoji watuhumiwa.

Kwa vile mauaji yalihusu mambo ya kishirikina ni dhahiri walengwa wakuu wangekuwa waganga wa kienyeji ingawa walikuwako na wengine pia.

Ingawa lengo lilikuwa zuri, utekelezaji ulikuwa mbaya.

Baadhi ya waliofanya mahojiano hayo walivuka mipaka ya utaratibu uliokubalika wa kuhoji watuhumiwa. Yakatokea mateso ya binadamu kinyume cha sheria, na watuhumiwa wengine wakafariki dunia. Mwinyi hakujua mpaka Mwalimu Nyerere alipopata taarifa hizo na kuunda tume ya uchunguzi.

“Ingawa binafsi sikuhusika na mateso na mauaji hayo, nikajihisi ninao wajibu wa kujiuzulu ili kulinda heshima ya Serikali na Rais Nyerere,” asimulia.

Jumamosi ya Januari 22, 1977 Mwinyi alimwandikia Mwalimu Nyerere barua ya kujiuzulu. Mwalimu naye alikubali kujiuzulu kwake. Siyovelwa naye alijiuzulu sambamba na wakuu wa mikoa hiyo ya Mwanza na Shinyanga.


Ubalozi Misri

Kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi. Baada ya muda, Mwinyi aliitwa na Mwalimu Nyerere nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam. Walipokutana, Mwalimu alimwambia: “Hassan, nimekuita. Nimeongea na Ben (Benjamin William Mkapa, Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo). Tumeafikiana tukupeleke Nigeria ukawe Balozi wetu huko.”

Hiki ni kipindi ambacho uhusiano wa Tanzania na Nigeria ulikuwa unarejeshwa baada kuvunjika pale Tanzania ilipotambua Jimbo la Biafra kuwa Taifa huru lililojitenga kutoka Nigeria.

Baada ya muda, Mwalimu alimwita tena. Akiwa na wasiwasi kuwa huenda Mwalimu ameghairi kumteua kuwa balozi, alipofika Msasani kwa Mwalimu, Nyerere alimwambia, “Ben na mimi tumefikiri tena. Tumeona ni bora uende kuwa Balozi wetu Misri.”

Hivyo ndivyo Mwinyi alivyokuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri ambako alidumu kwa miaka minne hadi aliporejea nyumbani Oktoba 1981.

Mara baada ya kurejea, aliteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Baadaye alibadilishiwa wizara na kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, anayeshughulikia Muungano. Kwa kuwa ofisi ya wizara hiyo ilikuwa Zanzibar, ilimlazimu kuhamia Zanzibar.


Urais wa Zanzibar

Baada ya kilichotajwa kama kuchafuka hali ya hewa Zanzibar, Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi alijiuzulu Januari 29, 1984.

Baada ya tukio hilo, kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Januari 30, 1984, jina la Mwinyi likapendekezwa na kupita na hapo akawa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1985, Mwinyi aligombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 27, 1985, kura ilipigwa ya NDIYO au HAPANA. Matokeo yalitangazwa Ijumaa ya Novemba 1, 1985 kuwa kati ya waliopiga kura 5,181,999 (asilimia 74.95 ya waliojiandikisha). Waliompigia kura ya NDIYO walikuwa 4,778,114, waliopiga kura ya HAPANA walikuwa 215,626 na kura zilizoharibika zilikuwa 188,259.

Hivyo Mwinyi akatangazwa kuwa mshindi kwa asilimia 92.20.

Kufuatia ushindi huo, Novemba 5, 1985, Ali Hassan Mwinyi, akiwa na umri wa miaka 60, aliapishwa kuwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hadi anakabidhi kijiti kwa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Novemba 23, 1995, jina ambalo wengi walipenda kulitumia ni “Mzee Ruksa” kwa sababu alifungua mlango wa mageuzi ya kiuchumi na kidemokrasia nchini.