Waguswa na afya ya Rais Mwinyi, wamtakia pole

Muktasari:

  • Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alikuwa Rais wa Tanzania mwaka 1985 na alitumia wadhifa huo hadi mwaka 1995.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kutolewa taarifa ya kuugua kwa Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, viongozi wa umma na wanasiasa maarufu wamemtakia afya njema kiongozi huyo.

 Taarifa ya kuugua kwa kiongozi huyo ilitolewa jana usiku Februari 2, 2024 na Msemaji wa familia, Abdulla Ali Mwinyi aliyesema kiongozi huyo amepelekwa hospitali akiugua maradhi ya kifua.

Hivyo kutokana na ushauri wa daktari wake, Abdulla amesema familia imeona ni vema apate faragha akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.

“Tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie shifaa ya haraka mzee wetu pamoja na wagonjwa wengine wote wanaokabiliwa na maradhi mbalimbali," amesema.

Baada ya taarifa hiyo, aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi kupitia ukurasa wake wa Instagram ameweka picha ya kiongozi huyo mstaafu akiandika, “Mwenyeezi Mungu mwingi wa rehma akujaalie shifaa, upone maradhi yanayokusibu, mzee wetu, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi. Unazo dua zetu. Amiin.”

Kiongozi mwingine ni aliyewahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose Bhanji aliandika  kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwa ameweka picha ya Rais mstaafu Mwinyi, “Mungu akufanyie wepesi Baba! Tunakupenda na kukuombea urejee kwenye afya yako.”

Mwingine ni Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa naye kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika,“Tuungane kumuombea Mzee wetu Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili apone haraka. Mwenyezi Mungu ashushe uponyaji na awape maarifa madaktari wetu, ili wakomeshe maradhi yanayomkabili.”