Mwinyi augua, ashindwa kuhudhuria mkutano wa CCM

Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi

Muktasari:

  • Wakati CCM kikiendelea na mkutano mkuu wa 10, Mwenyekiti wa chama hicho Rais Samia Suluhu Hassan amesema Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi ameshindwa kuhudhuria mkutano huo kutoka na kuugua akiwa Dodoma.

Dodoma. Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ameshindwa kuhudhuria mkutano wa 10 wa CCM baada ya kuugua mafua makali akiwa tayari yuko jijini Dodoma.


Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu leo Desemba 6, 2022 wakati akisoma salamu zake katika mkutano mkuu wa 10 unaoendelea katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.


Amesema Mwinyi ameshukuru kwa kumuwezesha kwenda safari ya matibabu na kurudi salama.

“Lakini naomba radhi kwa kutoweza kushiriki katika mkutano wa CCM leo kutokana na kushikwa na mafua makali, japokuwa niko tayari hapa Dodoma,” Rais Samia amemnukuu Mzee Mwinyi.

Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete

Pia, Rais Samia alisema salamu za Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete akieleza kusikitika kukosa mkutano huo.

Amesema Kikwete amesema hakuweza kushiriki kwa kuwa yuko nchini Ufaransa na kwamba atahakikisha kesho atakuwa kwenye mkutano huo.