Rais Samia awapa ujumbe CCM

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia azungumzia chaguzi za chama hicho zilizofanyika na zitakazofanyika leo baadaye akisema zina lengo la kuimarisha mshikamano na umoja wa CCM, awataka wajumbe mkutano mkuu kukubali mapendekezo ya halmashauri kuu.

Muktasari:

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia azungumzia chaguzi za chama hicho zilizofanyika na zitakazofanyika leo baadaye akisema zina lengo la kuimarisha mshikamano na umoja wa CCM, awataka wajumbe mkutano mkuu kukubali mapendekezo ya halmashauri kuu.

Dar es Salaam.  Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan amesema uchaguzi wa chama hicho unaofanyika leo ni nyenzo ya kuimarisha umoja, mshikamano na nguvu ya chama hicho tawala kilichominiwa na umma kuongoza nchi.

Amewataka wanachama wa CCM waliochaguliwa na wanaogombea katika uchaguzi utakaofanyika baadaye kutambua kwamba lengo la uchaguzi sio kutafuta ushindi wa mtu mmoja mmoja bali ni mkakati wa kujiimarisha na kujipanga kwa ajili ya kutafuta ushindi wa chama hicho katika chaguzi zijazo.

Ametoa kauli leo Jumatano Disemba 7, 2022 wakati akifungua mkutano mkuu wa 10 wa CCM unaondelea Jijini Dodoma katika ukumb wa Jakaya Kikwete. Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe 1928 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na Zanzibar.

“Tuna uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025, wote walioteuliwa kugombea nafasi walizoomba ni washindi kwa sababu chama kimewaamini kuwa yeyote angechakuliwa huku nyuma na leo ni mwanachama thabiti angeongeza nguvu yake kukijenga chama.

“Lakini kwa sababu ya uchache wa nafasi ni vigumu wote kuchaguliwa, kwa kutambua hilo na kupanua wigo wa ushiriki wa wanachama, halmashauri kuu imekuja na mapendekezo katika kufanikisha jukumu lililopo mbele yetu la kutafuta ushindi wa CCM mwaka 2024 na 2025,” amesema.

Samia ambaye ni Rais wa Tanzania amesema halmashauri kuu ya chama hicho, imepeleka mapendekezo katika mkutano mkuu wa CCM yanayolenga kuongeza nafasi za wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM taifa kutoka 15 za Tanzania bara hadi 20 hivyo hivyo kwa Zanzibar kutoka 15 hadi 20.




Pia, kuongeza idadi ya wajumbe wa halmashauri ya CCM wanaoteuliwa wanaopatikana chini ya Ibara 102 (12) E ya Katiba ya CCM ya 1977 toleo la 2022 kutoka wateuliwa saba hadi 10.

“Matarajio yangu wajumbe wote wa mkutano mkuu huu wa 10 mtatambua dhamira njema ya halmashauri kuu ya CCM kuhusu mapendekezo haya na mtayapitisha ili kuzidi kukipa chama sura mpya ya utekelezaji bora wa mipango yake,”

Awali kabla ya kuanza kutoa hotuba ya ufunguzi, mwenyekiti huyo aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuwa watulivu wakati wote wa kikao hicho kikiendelea.

“Jana kucha mmeomba kura jana leo nataka utulivu wa kutosha, makatibu wa mikoa naomba mtulize watu wenu, vijana wa CCM mnatoa huduma anayesimama bila sababu naomba mtoeni nje,”amesema Rais Samia