Rais Samia: Wajumbe tuosheni

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono na kuwasalimia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho alipokuwa akiwasili katika ukumbi kwa ajili ya kuongoza mkutano huo jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan ameomba kura kwa nafasi yake na kuwaombea wagombea wengine waliokuwepo madarakani akitaka wawaoshe watakate ili warudi kukitumikia chama.

Dodoma. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan ameomba kura kwa nafasi yake na kuwaombea wagombea wengine waliokuwepo madarakani akitaka wawaoshe watakate ili warudi kukitumikia chama.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Desemba 7, 2022 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM unaofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jiji Dodoma.

🔴#LIVE: Mkutano mkuu CCM

Katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais Samia amesema 'mwosha huoshwa' hivyo ni zamu ya wagombea wa nafasi ya juu katika chama hicho.

"Nilipohutubia mkutano Mkuu wa uchaguzi wa UWT niliwaambia kuwa, mwosha huoshwa, sisi tumeosha wenzetu kuanzia ngazi ya mashina Sasa ni zamu yetu kuoshwa, lakini naomba mtuoshe tutakate turudi kukitumikia chama chetu," amesema Rais Samia.

Kauli ya Mwenyekiti Samia huenda ikawagusa viongozi wa juu waliokuwepo madarakani ndani ya CCM ambao wameomba kugombea tena.

Miongoni mwao ni Rais Samia ambaye amependekezwa kutetea nafasi ya Mwenyekiti,Abdulrahman Kinana ambaye anatetea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wakati Shaka Hamdu Shaka na Christina Mndeme wakimenyana kugombea Viti 40 vya Ujumbe wa NEC.

Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete (kushoto) akijadiliana jambo na Mjane wa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli walipohudhuria Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM unaofanyika leo, jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Jumla ya wajumbe 1928 wamehudhuria mkutano huo na wajumbe 6 pekee ndiyo hawakushiriki kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo.

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana (katikati) akisalimiana na Spika Mstaafu, Job Ndugai walipohudhuri Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM unaofanyika leo, jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Wanachama 374 kutoka CCM wamejitokeza kuomba nafasi 40 za ujumbe wa NEC ambazo zimegawanyika kutoka Tanzania Bara 20 na Zanzibar 20 kutokana na mapendekezo ya Halmashauri Kuu ambayo wajumbe wameridhia.