Mwili wa mwanamke aliyeuwawa kwa kupigwa risasi na mumewe wazikwa

Picha ya Swalha Salum aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mmewe, Said Oswayo jijini Mwanza

Muktasari:

Mwili wa mkazi wa Busweru wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Swalha Salum aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mumewe kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi umezikwa leo katika makaburi yaliyoko Kirumba mkoani Mwanza.

Mwanza. Mwili wa mkazi wa Busweru wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Swalha Salum aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mumewe kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi umezikwa leo katika makaburi yaliyoko Kirumba mkoani Mwanza.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na mamia ya wakazi wa mkoa wa Mwanza huku vilio, simanzi na majonzi yakitawala wakati mwili huo ulipopelekwa makabulini.

Swalha alipigwa risasi saba usiku wa Jumamosi Mei 28, 2022 na mumewe, Said Oswayo wakiwa nyumbani kwao katika mtaa wa Mbogamboga kata ya Busweru wilayani humo baada ya kuibuga ugomvi kati yao.

Siku mbili baada ya kutekeleza mauaji hayo huku juhudi za maofisa wa Jeshi la Polisi wakimtafuta, Jumatatu Mei 30,2022 mwili wa mtuhumiwa wa shambulio hilo, Said Oswayo nao ulionekana ukielea kwenye maji katika ufukwe wa Rock Beach jijini Mwanza huku ndugu wakithibitisha kuwa ni mwili wa ndugu yao.

Mwili wa Swalha umezikwa leo mchana katika makaburi ya Kirumba baada ya kusomewa kisomo na kuswaliwa katika msikiti uliopo Kirumba mkoani humo huku siku rasmi ya mazishi ya mwili wa mmewe ukiwa bado haijajulikana.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Mairi Makori amesema maofisa wa jeshi hilo walipata bastola moja yenye risasi nane katika ufukwe wa Rock Beach ambayo inadaiwa kutumiwa na mume wa mwanamke huyo kufanya mauaji kisha kujiua.

Amesema hadi sasa hajapitia ripoti ya daktari kuhusiana na uchunguzi wa miili ya wanandoa hao kutokana na kutingwa na majukumu mengine.

"Sasa hivi niko wilayani Kwimba kwenye majukumu mengine lakini nimepata taarifa kuwa mwanamke ameshazikwa. Nikirejea ofisini nitaipitia ripoti hiyo na kutoa taarifa," amesema Makori