Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwili wa mwanamke wakutwa ukielea bwawani

Mwili ukiwa umeopolewa kwenye bwawa la Mbimba wilayani Mbozi ukipakiwa kwenye gari kuelekea kuhifadhiwa hospitali

Songwe. Mwili wa mwanamke mmoja ambaye hajafahamika, umekutwa ukielea katika Bwawa la Mbimba, linalotumika kwa shughuli za umwagiliaji kando ya Barabara ya Tanzania - Zambia wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe.

Mwili huo umekutwa umeharibika na uliopolewa jana Jumanne Julai 30, 2024 jioni na haijulikani mwili huo kama umetupwa au mtu huyo alitumbukia mwenyewe bwawani humo.

“Baada ya kuuona, wananchi walitoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Songwe ambao walifika na kuuopoa,” amesema Baka Mwangosi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbimba alipozungumza na Mwananchi Digital kuhusiana na tukio hilo leo Jumatano Julai 31, 2024.

Mwangosi ameliomba Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika eneo hilo kwa kushirikiana na wananchi.

“Hatujui kama huyu mtu alitumbukia mwenyewe kwenye hili bwawa au kuna watu wamemtumbukiza, bado ni kitendawili,” amesema Mwangosi.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Songwe, Joseph Kapange amesema walipokea taarifa hizo jana jioni kutoka kwa wananchi.

Amesema walipofika eneo la tukio, walibaini mwili huo ni wa mwanamke na ulikuwa umeharibika mdomoni.

Hata hivyo, amesema hili ni tukio la pili kutokea katika bwawa hilo, “Mwaka jana pia tuliopoa mwili wa mwanamke mwingine ambaye pia haikujulikana ni mkazi wa wapi na hata wenyeji wa hapa hakuna aliyekuwa anamfahamu.”

Mmoja wa mashuhuda na mkazi wa Mbimba, Joseph Mwazembe amesema tukio hilo limewashtua na linaibua hofu kwa wananchi.

“Mwaka jana pia kuna maiti ya mwanamke ilitolewa kwenye bwawa hili, sasa hii inaleta maswali halafu siyo watu wanaoishi hapa kwa sababu hata huyo wa mwaka jana maiti yake haikutambuliwa na sijui ilizikwa na Serikali au ndugu zake walipatikana hakuna anayejua,” amesema Mwazembe.

Naye Mariam Hamis amesema kuna haja sasa ya wananchi nao kulilinda bwawa hili.

“Hii ni maiti ya pili sasa, Serikali nayo itusaidie kulitazama hili, hatutaki kuona bwawa hili sasa linatumika kama eneo la kutupa miili ya watu,” amesema hamis.

Kapange amesema mwili wa mwanamke huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na ametoa wito kwa wananchi ambao wamepotelewa na ndugu kufika hospitalini hapo kuutambua mwili huo kama ni wa ndugu yao.

Mbali na eneo hilo Julai 22, 2024, jijini Dodoma miili ya wanawake wawili katika Mtaa wa Chinyika iliokotwa huku mmoja ukionekana kujeruhiwa na kitu chenye ncha kali.

Kwa mujibu wa mashuhuda, mwili huo ulioonekana kujeruhiwa na kitu chenye ncha kali, ulikutwa ukiwa umefungwa katika nailoni, boksi na kiroba.

Tukio hilo lilitokea ikiwa ni miezi michache tangu mwili wa mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 30 na 40 uokotwe ukiwa kando mwa barabara kuu ya Moshi - Arusha, eneo la Kwa Msomali, kitongoji cha Darajani

Kitongoji hicho ambacho kipo katika kijiji cha Sanya Station, kipo wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.

Tukio hilo lilitokea Januari 28, 2024 huku mwanamke huyo ambaye hakujulikana wala eneo alikouawa, ukiwa umeharibika kiasi cha kutoa wadudu.

Pia Februari 24, mwaka huu mwili mwingine wa mwanamke aliyetambulika kwa jina la Josephine Mngara (27), mkazi wa Mtemboni, Mji mdogo wa Himo, Mkoani Kilimanjaro uliripotiwa kuokotwa huku ikidaiwa kuwa aliuawa na mpenzi wake na kisha mwili wake kuchomwa moto.


Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.