Mzanzibar anyakua 30 milioni mashindano ya Qur’an Afrika Mashariki

Muktasari:

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka wazazi na walezi kusimamia maadili ya vijana wao ili kuwa na mustakabali mwema katika maisha yao.

Unguja. Mahmoud Kassim Nassor (20) kutoka Zanzibar ameibuka mshindi katika mashindao ya kuhifadhi Qur’an ya Afrika Mashariki na kupewa zawadhi ya Sh30 milioni baada ya kupata alama 99.5.

Mshindi wa pili katika mashindano hayo yaliyoshirikisha nchi saba, ni Abdul Rahman Papa Said (19) kutoka Comoro aliyepata alama 98.75 na kupewa hundi ya Sh20 milioni huku mshindi wa tatu Abdul-rahman Mussa (14) kutoka Kenya amepewa hundi yenye thamani ya Sh10 milioni baada ya kupata alama alama 97.

Nchi zingine zilizoshiriki mashindano hayo ni Uganda, Tanzania Bara, DR Kongo na Zambia.

Akizungumza katika mashindano hayo yaliyofanyika uwanja wa New Amani Complex leo Jumamosi Machi 30, 2024, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema mashindano hayo yatasaidia kuitangaza vyema Tanzania, huku akiwasihi wananchi kusoma Qur'an kwa wingi na kuunga mkono jitihada za taasisi zinazoshghulika kuhifadhi Quran.

Pia ameitaka ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kuendelea kusimamia malezi bora kwa watoto na vijana kujifunza vitabu vitukufu ili kunusuru Taifa kupata mporomoko wa maadili.

Hata hivyo, amesema jukumu la kusimamia maadili si la walimu pekeee bali ni la wananchi wote hivyo amewataka wazazi na walezi nao kusimamia maadili ya vijana wao ili kuwa na mustakabali mwema katika maisha yao.

"Kipekee niwashukuru vijana wa Zanzibar kutuwakilisha vyema kwa kujiamini kushindana na washiriki kutoka nje ya Nchi."amesema Dk Mwinyi

Naye Shekh Mziwanda Ngwali Ahmed kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar amesema si mara ya kwanza Zanzibar kuandaa mashindano kama hayo, lakini kwa mwaka huu  mashindano hayo ni ya aina yake kutokana na ushiriki wa mataifa mengi.

Sheikh Mziwanda amesema washiriki wa mashindano hayo ya kimataifa ni wanaume wenye umri kati ya miaka 13 hadi 23.

Mwenyekiti wa mashindano hayo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Ramadhan Bukini amesema lengo kuu la mashindano hayo ni kuwaunganisha waumini wa dini ya Kiislam wa nchi mbalimbali kupitia Qur-an.