Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzazi fanya haya mtoto akiwa likizo

Dar es Salaam. Tunapoelekea kumaliza likizo, kabla ya kumrejesha mtoto shuleni kuna hatua kadhaa muhimu ambazo mzazi au mlezi anapaswa kuchukua ili kuhakikisha mwanafunzi anarudi kwa mafanikio na anajiandaa vizuri kwa masomo.

Baadhi ya mambo ambayo anaweza kufanya ni kurekebisha ratiba ya kulala na kuamka, ili kuwarudisha watoto kwenye utaratibu wa shule. Ni muhimu pia kuhakikisha mtoto amepata vifaa vyote muhimu ikiwemo sare, vitabu na vifaa vingine vinavyohitajika. Hii itamsaidia kujisikia tayari na kujiandaa kwa masomo.

Si hivyo tu, kuna haja ya kumsisitiza mtoto umuhimu wa elimu kwa kuweka matarajio chanya kwa kuwa shuleni ni mahali pa kujifunza na kukuza ujuzi.

Mbali ya hayo, kuna haja ya kuweka malengo ya kuyafuatilia katika masomo yao, hili litawapa motisha zaidi. Mzazi au mlezi anawajibika kuhakikisha mtoto amepata muda wa kufanya kazi za shule, kusoma vitabu, au kufanya shughuli nyingine za kujifunza.


Uchaguzi wa shule

Baadhi ya watoto wanaokwenda kuanza masomo ya msingi na sekondari, huku wengine wakihamishwa kutoka shule moja kwenda nyingine. Katika kuhakikisha mtoto anapata shule nzuri, Josephina Kiwele, ambaye kitaaluma ni mwalimu anashauri mzazi azingatie mazingira ilipo kama ni rafiki kwa mwanafunzi kujifunza, ufundishaji na maadili.

Anasema hilo litamfanya mzazi kuona tofauti ya watoto wanapokuwa nyumbani na shuleni.

"Tunapeleka watoto shule binafsi kwa sababu tunaangalia anapata nini, huwezi kumpeleka ambayo mazingira yake ni hovyo, ufundishaji ni shida na ukiangalia unalipa pesa," anasema.

Anasema zipo shule zenye mazingira mazuri lakini ufundishaji si mzuri na hazisaidii watoto kwenye maadili.

Nicodemus Shauri, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Maarifa ni Ufungo anasema wazazi wanatakiwa kuzingatia ukaribu wa shule, hasa kwa wanaoanza shule za msingi.

"Ukaribu wa shule unamsaidia mtoto katika usalama wake, wapo wanaosoma mbali wanakutana na misukosuko njiani ikiwapo kupoteza au kutumia nauli, hivyo inasababisha mtoto kusumbuana na makondakta anaposaka usafiri," anasema na kuongeza:

"Shule za binafsi wana magari lakini watoto wanatumia muda mwingi njiani na kusababisha kuchoka kwa sababu ya kutoka nyumbani mapema.”

Anasema mtoto kusoma mbali ni gharama kwa mzazi na itampa wakati mgumu kumfuatilia kwa karibu.

Shauri anasema jambo lingine la kuzingatia ni ufundishaji akieleza:

"Kuna haja ya mzazi kufuatilia ufundishaji wa shule maana zipo zinazokaririsha na zinafanya udanganyifu kwenye mitihani ili kuvutia wateja ni muhimu kufuatilia jambo hilo."

Richard Temu, mkazi wa jijini Dae es Salaam anasema wazazi wengi wanaangalia matokeo ya darasa la nne, la saba na kidato cha nne lakini hiyo haitoshi kwani usalama na uendelevu wa mtoto ndiyo suala muhimu zaidi shuleni.

"Shule si adhabu wala mateso, mtoto anatakiwa kusoma kwa furaha ili aone ni kitu anachokipenda, tumekuwa na tabia ya kupeleka watoto shule za mbali kutokana na ubora lakini ni mateso kwa mtoto," anasema Temu.

Anashauri wazazi waangalie masharti yanatolewa na shule ikiwapo kutembelea watoto zaidi ya siku ambazo zimewekwa na shule.

"Shule zinaweka masharti ya kutembelea watoto lakini ni muhimu pia kushtukiza safari ya shule ili kuona maendeleo ya mtoto kwa sababu akibadilika inakuwa rahisi kumrekebisha," anasema.


Mwaka mpya wa masomo

Wakati hayo yakielezwa yafanyike kwa upande wa mzazi au mlezi, wamiliki wa shule binafsi na wasimamizi wa zile za serikali wametakiwa kufanya tathmini na kuboresha miundombinu ikiwemo ya madarasa, maabara, walimu, vitabu na vyoo.

Maboresho hayo yafanyike ili kuendana na ongezeko la idadi ya wanafunzi linaloshuhudiwa kila mwaka, huku wakieleza kuwa ni vyema kama nchi kujiandaa ili kukabililiana nalo.

Shule za sekondari zinajiandaa kupokea wanafunzi milioni 1.2 watakaojiunga kidato cha kwanza Januari 8, mwakani.

Akizungumza na gazeti hili, Alistidia Kamugisha ambaye ni mdau wa elimu alisema wanatamani kuona idadi ya walimu ikiongezwa walau kufikia wastani ambao mwalimu anaweza kuwafundisha wanafunzi na akaeleweka.

Hiyo itawafanya wanafunzi kuhudhuria shuleni na kuelewa kile wanachofundishwa na si kuhudhuria tu na kuondoka wakiwa hawana kitu kichwani.

“Tuongeze pia madarasa, juhudi zimefanyika katika kupanua shule, kuongeza idadi ya madarasa katika baadhi ya shule kwa kuzifanya kuwa za ghorofa lakini, tuongeze zaidi ili mazingira ya shule kwa mwanafunzi yawe ya kuvutia,” alisema Alistidia.

Suala la njaa kwa wanafunzi pia ni jambo ambalo linaweza kufanya watoto wengi kukosa hamu ya kukaa shuleni, akitaka juhudi zifanyike ili kuwasaidia kuondokana na tatizo hilo linaloweza kuchangia mdondoko wa wanafunzi.

“Mabweni kwa wanafunzi, tusiangalie mijini, kuna wanaotoka mbali vijijini, wanatembea umbali mrefu, kuna wanafunzi wanatembea hadi kilomita saba kufika shuleni, tuangalie hili. Lisipofanyiwa kazi kutakuwa na mdondoko maana mtoto akishinda na njaa shuleni, akatembea umbali mrefu inamkatisha tamaa,” alisema.

Kuhusu utoaji wa chakula shuleni, Oktoba 25, mwaka huu Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia Elimu, Dk Charles Msonde alisema kushinda njaa kwa wanafunzi ni moja ya sababu inayochangia kuwapo kwa utoro wa wanafunzi.

Kwa kulitambua hilo, Serikali ilianzisha mkakati wa upatikanaji wa chakula shuleni. Mkakati huo ulifanyika kupitia mikataba ya lishe waliyosaini wakuu wa mikoa ili waweze kushirikiana na viongozi walio chini yao pamoja na wazazi katika kufanikisha upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi ili waweze kujifunza kikamilifu.

“Mtoto anapokuwa ameshiba anakuwa na hamu ya kuendelea kubaki shuleni, kujifunza na kuelewa lakini anapokuwa na njaa ni ngumu kuelewa. Sisi tu watu wazima tukishinda kutwa nzima bila kula kazi haziendi,” alisema.

Utekelezaji wa mikataba hii ya lishe unahusisha viongozi wa ngazi mbalimbali hadi wale wa mitaa ili kuhakikisha kila mmoja anafikiwa na kufahamu umuhimu wa chakula kwa watoto shuleni.

Muhanyi Nkoronko, mdau wa elimu alisema ni vyema uwekezaji zaidi katika sekta ya elimu ukafanyika ili kuondoa changamoto zinazoikabili.

Hilo liende sambamba na umaliziaji wa miundombinu, ikiwemo madarasa na maabara zilizoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.

“Walimu ni muhimu, ruzuku pia kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari iongezwe, kuongezwa kwa ruzuku hii kunaisaidia kupunguza baadhi ya changamoto zinazozikabili shule mbalimbali,” alisema Nkoronko.

Ameishauri Serikali kuongeza kasi ya ufundishaji walimu ili kuendana na mabadiliko ya mtalaa uliofanywa na Serikali ili iweze kuendana na kasi ya dunia.

Mtalaa mpya wa masomo anaouzungumzia Nkoronko utaanza kutumika Januari mwakani utawahusu wanafunzi walio darasa la tatu.