Mzee aliyedaiwa kupelekwa mochwari akiwa hai, afariki
Baadhi ya waombolezaji wakiwasili nyumbani kwa Mzee Simon Macha eneo la Mtaa wa Kwa Sawaya, Majengo Manispaa ya Moshi ambaye taarifa za kifo chake zilizua taharuki, baada ya taarifa za awali kudai kuwa mzee huyo kafariki na watu kuweka msiba nyumbani hapo, lakini baadaye zililetwa taarifa nyingine kwamba hajafa.
Muktasari:
- Leo asubuhi waomboleza waliokuwa nyumbani waliambiwa mzee huyo hajafariki dunia kama ilivyoelezwa jana.
Moshi. Ni tukio la kutatanisha. Hii ni baada ya mzee mmoja aliyejulikana kwa jina la Saimon Macha juzi akiwa hospitalini KCMC alikokuwa amelazwa, kudaiwa amekufa na baadaye ikabainika kuwa bado yuko hai akiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.
Baada ya wanafamilia kupata taarifa za kufariki kwa mzee huyo, kama ilivyo ada waliweka msiba nyumbani kwake, Mtaa wa Kwa Sawaya, Kata ya Majengo, wilayani Moshi mjini.
Hata hivyo, jana asubuhi waomboleza waliokuwapo nyumbani hapo waliambiwa mzee huyo hajafariki dunia kama ilivyoelezwa juzi.
Akizungumzia tukio hilo jana, shuhuda aliyelala msibani hapo alisema; “Tulipata taarifa za msiba wa mzee Macha juzi mchana kutoka kwa ndugu, tukafunga maturubai hapa na msiba ukaanzishwa, lakini jana asubuhi zikaja taarifa kuwa mzee Macha hajafa yuko hai ila amelazwa ICU.”
Alisema baada ya taarifa hizo, waombolezaji waliokuwa wamejikusanya nyumbani hapo kwa mshangao mkubwa ikabidi waondoke na maturubai yakafunguliwa.
Alieleza kuwa taarifa za kuwa mzee Macha amefariki dunia jana, wamepewa na ndugu ambao walienda hospitali kumuona mchana na kukuta amefariki dunia kweli.
“Taarifa ya pili ya Mzee Macha kufariki, tumepewa jioni ya jana na ndugu ambao walienda KCMC kumuona, ndiyo wamekuta amefariki kweli, tumebaki tunashangaa, ndiyo tunaendelea na msiba tena,” alisema shuhuda huyo.
Mmoja wa wanafamilia ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa bado hawajamteua msemaji alisema, “Maneno yamekuwa mengi sana, hata hivyo sisi kama familia hatuna malalamiko yoyote dhidi ya hospitali na wala hatumlaumu mtu.”
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseo alisema kilichotokea ni mkanganyiko wa taarifa kwa ndugu hao, kwani mgonjwa alipofikishwa hospitalini hapo ubongo wake ulikuwa tayari umeshakufa.
"Huyu mgonjwa aliletwa kwetu ubongo wake ukiwa umekufa, kitaalamu ubongo ukifa moyo unaweza ukawa unapiga na hata huyo mtu mnaweza kukaa naye hata miaka 10, anakuwa ni nusu mfu.
"Ubongo ukisimama ni Mungu mwenyewe ndiye anabaki kuwa mwamuzi, wataalamu hufikia mahala wanakuwa hawana uwezo tena wa kuuamsha, kwa hiyo alikuja tayari ubongo umelala,” alisema.
Kuhusu mgonjwa kupelekwa mochwari akiwa hai, Chisseo alisema si kweli. “Wala hakupelekwa mochwari kama taarifa zilivyovuma, pale wodini hata mke wake hakuwepo, na baada ya mgonjwa kugundulika ubongo umesimama alipelekwa moja kwa moja ICU, na si chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema.
Alisema hata ndugu wa marehemu walielezwa kuhusiana na tatizo la ubongo kusimama kufanya kazi. “Na ili kuondoa mashine ya kupumulia ni lazima wataalamu wawili wakutane wasaini na ndugu wasaini, kisha wanaelezwa kwamba wanaizima mashine, lakini jana wakati utaratibu huo unataka kufanyika, ndugu hawakuwepo kwa hiyo haikufanyika.
"Asubuhi kukatokea sintofahamu huko kwenye familia kwamba sisi tumesema mgonjwa ni mzima, kitu ambacho sio kweli kama hospitali hili ni jambo la kitaalamu sana.
“Hapa naweza kusema ni mawasiliano kati ya msimamo wa kitabibu na jamii ilivyopokea taarifa hiyo, ndiyo yakazushwa haya yaliyozuka,” alisema.