Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzee wa kanisa azikwa, Katibu wa jimbo ataka Serikali kukagua madereva

Mwili wa mzee wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Leban Kweka (50) ukitolewa kanisani kwa ajili ya Kupelekwa nyumbani kuzikwa katika makaburi ya familia.

Muktasari:

  • Mchungaji Munis na mzee wa kanisa, Laban walifariki dunia kwa ajali ya gari Agosti 4, 2024 baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongwa na basi la Shabiby wakati akikata kona kuingia Usharika wa Kimashuku ambako anaishi.

Hai. Wakati mamia ya waombolezaji wakiaga mwili wa Mchungaji  Kiongozi wa Usharika wa Kimashuku, Kantate Munis (42) na mzee wa kanisa hilo, Laban Kweka (50), Katibu wa Jimbo la Hai Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT), Mwinjikisti Ernest Massawe ameiomba Serikali inapokagua vyombo vya moto iwakague na maderava ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

Amesema ajali nyingi zinazotokea na kusababisha vifo na hata majeruhi, hutokana na uzembe wa maderava kutozingatia sheria za usalama barabarani.

Mchungaji Munis na mzee Laban walifariki dunia kwa ajali ya gari Agosti 4, 2024 baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka kwenye uimbaji Usharika wa Gezaulole wilayani Hai, kugongwa na basi la Shabiby wakati akikata kona kuingia Usharika wa Kimashuku anakoishi.

Mzee Laban amezikwa leo Alhamisi Agosti 8, 2024 katika makaburi ya familia yaliyopo eneo la Kimashuku, Kata ya Mnadani, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, huku mwili wa Mchungaji Munis ukisafirishwa kwenda kijijini kwao Kisamo Old Moshi, Wilaya ya Moshi kwa maziko yatakayofanyika kesho Ijumaa Agosti 9, 2024.

Wakati miili hiyo ikiagwa kanisani hapo, vilio na simanzi vilitawala kwa waombolezaji, huku wengine wakishindwa kujizuia na kuanguka.

Katibu wa Jimbo la Hai, Mwinjikisti Massawe, amesema suala la ajali linaweza kuepukika endapo Serikali itachukua hatua stahiki za kuhakikisha madereva wanazingatia sheria za usalama barabarani.

Amesema ajali nyingi zimeacha majonzi katika baadhi ya familia na majeraha yasiyofutika.

"Tunaomba vyombo husika kuhakikisha wanapokagua magari wawakague na madereva kwa sababu ukiangalia mazingira mahali ajali hii ilipotokea ni mtu aliyekosa heshima, angefuata sheria za barabarani ile ajali isingetokea," amesema Massawe.

Akihubiri katika ibada hiyo, Mchungaji David Shao ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira kitivo Cha Theolojia, ametaka msiba huo kuwa fundisho kwa mtu kujiandaa kwa kutenda mema, akitambua ipo siku ataondoka duniani.

Aidha, ametumia pia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuishi maisha ya kuacha alama, ili kukumbukwa pindi watakapoondoka duniani.

"Wenzetu hawa wameondoka lakini wameacha alama, kuna vitu mkiviona mtamkumbuka Mchungaji Kantate, kuna alama ya watoto wake, alama ya kazi na hata mahubiri yake, lakini pia kuna vitu mkiviona mtamkumbuka mzee Laban, bado watakuwa wanaishi mioyoni mwetu," amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wachungaji wanawake, Anna Makyao amewasihi wafiwa kumtazama Mungu zaidi.

"Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya Mchungaji Kantate na mzee Laban, Mungu alitupa hawa kama watumishi, walitumika vyema na walifariki wakati wakitoka kwenye majukumu ya utumishi," amesema.

Ametoa pole kwa Mchungaji Israel Moshi, watoto, familia ya mzee Laban na wote walioguswa na msiba huu.