Mzee wa miaka 62 adaiwa kumbaka mwanafunzi shule ya msingi

Muktasari:

Mkazi wa Kibaha Mkoa wa Pwani, Maxmilian Malima (62) amepandishwa kizimbani akikabiliwa na tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Kilangalanga mkoani humo.


Kibaha. Mkazi wa Kibaha Mkoa wa Pwani, Maxmilian Malima (62) amepandishwa kizimbani akikabiliwa na tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Kilangalanga mkoani humo.

Akisoma maelezo ya awali leo Jumanne Desemba  13, 2022 mwendesha mashtaka wa Serikali, Rose Ishabakaki akisaidiana na Eliza Olomi mbele ya hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Fahamu Kibona amesema kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo kwa nyakati tofauti tofauti mwezi Julai na Octoba 2022.

Amesema kuwa siku moja kati ya mfululuzo wa matukio hayo  mtuhumiwa huyo alimuita Mwanafunzi huyo wakati akielekea shuleni na kumtuma dukani akamnununulie mahitaji na aliporejea alimvutia ndani ya nyumba yake kísha kumfanyia kitendo hicho.

"Siku ya tukio mtuhumiwa alimuita Mwanafunzi huyo wakati akielekea shuleni akamtuma dukani na aliporejea alimvutia ndani kwake na kumbaka," amesema.

Amesema kuwa kutokana na hali hiyo ilibainika na baadaye kukamatwa kufikishwa Polisi na hata kwenye mahakama hiyo.

Hata hivyo mshtakiwa huyo amekana kuhusika na tuhuma hizo na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.

Anayesikiliza shauri hilo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha mkoani humo, Fahamu Kibona ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 4,2023 itakapoendelea kwa hatua zingine.