Mzindakaya azikwa akikumbukwa kwa uzalendo

Muktasari:
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga amesema mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Chrisant Mzindakaya ni tunu ya uzalendo uliotukuka inayotakiwa kuenziwa na Watanzania kwa sababu bado inahitajika kwa ustawi wa Taifa.
Sumbawanga. Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga amesema mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Chrisant Mzindakaya ni tunu ya uzalendo uliotukuka inayotakiwa kuenziwa na Watanzania kwa sababu bado inahitajika kwa ustawi wa Taifa.
Ameeleza hayo leo Jumamosi Juni 12, 2021 katika ibada ya mazishi ya Mzindakaya iliyofanyika katika Kanisa la Kristo Mfalme lililopo Jimbo Katoliki la Sumbawanga mkoani Rukwa.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ibada hiyo ni Spika wa Bunge, Job Ndugai; mawaziri wakuu wastaafu, John Malecela na Mizengo Pinda; naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Godfrey Pinda; wabunge wa mikoa ya Rukwa na Katavi na wakuu wa mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe.
Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo Katoliki Mbeya amesema namna nzuri kwa Watanzania kumuenzi Mzindakaya ni kuendeleza na kudumisha yale yote mazuri aliyoyafanya wakati wa uhai wake.
"Namfahamu Mzindakaya kama mzalendo halisi alikuwa akiililia na kuitetea nchi kwa moyo wa dhati..., licha ya kushika nyadhifa mbalimbali hakuwa na majivuno wala dharau kwa mamlaka wala mtu yoyote kwa Taifa, ndio maana nasema ni urithi mkubwa kwa Taifa hili na tunu inayotakiwa kuenziwa,” amesema.
Akitoa salamu za Bunge, Ndugai amesema Taifa limempoteza mtu muhimu, mpigania maendeleo ambaye muda wote wa maisha yake aliutumia kulitumikia Taifa kwa unyenyekevu na upendo.
Ndugai amesema atashirikiana na mbunge wa Sumbawanga mjini (CCM), Aeshi Hilaly kuibana Serikali ili katika bajeti ya 2021/22 ijenge kwa kiwango cha lami Uwanja wa Ndege Sumbawanga ili kuwahudumia wananchi.
Naye Malecela amesema Mzindakaya alisaidia maendeleo ya Mkoa wa Rukwa na Taifa hasa wakati wa kutekeleza mradi wa kilimo cha mahindi.
"Sio tu alisimamia vizuri mradi wa kuhamasisha kilimo NA Rukwa kuwa miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wingi mazao, pia maendeleo unayoyaona leo hii katika mkoa huo ni matokeo ya mchango wake mdogo wangu Mzindakaya,” amesema Malecela.
Dk Mzindakaya alifariki dunia Juni 7, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo.
Amezikwa nyumbani kwake eneo la Kilimani kata ya Majengo mjini Sumbawanga.