Mzungu Michael Chain alivyoibua jina Mikocheni
Muktasari:
- Makala yanaangazia baadhi ya maeneo hayo ambayo majina yake yametoholewa kutoka katika Kiingereza.
Unadhani utohoaji wa maneno ya kigeni hasa yale ya lugha ya Kiingereza hufanywa kwenye msamiati wa pekee?
Watanzania wameenda mbali ya utohozi wa msamiati. Kuna maeneo kadhaa nchini, majina yake yana asili ya maneno ya Kiingereza.
Hapa tutaangazia baadhi ya maeneo hayo ambayo majina yake yametoholewa kutoka katika Kiingereza.
Kariakoo
Hujafika Jiji kuu la Dar es Salaam kama hujakanyaga eneo la Kariakoo ambalo ndilo kitovu cha biashara sio tu kwa jiji hilo bali kwa nchi.
Lakini unajua kama asili ya neno hilo ni maneno ya Kiingereza Carrier corps yaani vikosi vya wabeba mizigo/ wapagazi.
Historia kutoka vyanzo mbalimbali inaeleza kuwa miaka ya 1914 wakati wa vita vya kwanza vya dunia.. eneo hilo lilikuwa maskani ya wapagazi hao waliokuwa wakisambaza kwa miguu vifaa kwa wanajeshi wa Kiingereza
Kwa kushindwa kutamka neno hilo, wenyeji wakafanya utohozi wakalipa jina la Kariakoo, jina lililoendelea kutumika mpaka sasa
Cow ways ilivyozaa Kawe
Kawe ni eneo lingine maarufu jijini Dar es Salaam ambalo simulizi za kihistoria zinaeleza kuwa limetokana na maneno ya Kiingereza Cow ways yaani njia ya kupita ng’ombe.
Ni eneo ambalo wanyama hao walikuwa wakiswagwa kuelekea kilipokuwa kiwanda cha kuchakata nyama cha Tanganyika Packers.
Kwa kushindwa kulitamka, wenyeji wakaishia kuliita Kawe.
Aidha, Kawe kwa mujibu wa maelezo ya wavuti wa Wilaya ya Kinondoni, linanasibishwa pia na mwanamama aliyejukikana kwa jina la Bi Mwakawi aliyekufa na kuzikwa katika makaburi ya Mzimuni, miaka ya 1908 eneo linalotajwa kuwa ndio Kawe ya Kwanza.
Mikocheni
Eneo hili awali liliitwa kwa jina la Mzungu aliyekuwa akiitwa Michael Chain. Waswahili waliposhindwa kulitamka wakaishia kusema Mikocheni.
Chekereni
Mkoani Kilimanjaro kuna eneo linaitwa Chekereni. Kwa mujibu wa mwalimu mstaafu, Elisaria Mrema neno hilo linatokana na jina maneno ya Kiingereza ‘Check the rail’.
Kiboriloni
Vivyo hivyo kwa Kiboriloni analosema limetokana na maneno ya Kingereza Kibo alone na Kibo line. Kumaanisha kilele kimojawapo cha Kibo kilichopo kwenye Mlima Kilimanjaro.
New well
Kuna simulizi ya kihistoria inayoeleza kuwa Wilaya ya Newala iliitokana maneno New well (kisima kipya). Hata hivyo, ipo simulizi nyingine kuwa neno hilo lina asili ya lugha ya Kimakonde Niwaala, ambalo Mjerumani alishindwa kulitamka akaishia kusema Newala.
Sio Kiingereza pekee
Si maneno ya Kiingereza pekee, majina ya maeneo pia yapo yanayotokana na lugha nyingine. Kwa mfano, Dar es Salaam asili yake ni neno la Kiarabu Daarul salaam likimaanisha nyumba/dari ya amani au mahala pa salama.
Ni jina la uliokuwa mji uitwao Mzizima (eneo lenye neema au afya). Uliitwa Daarul salam baada ya ujio wa Sultan Sultani Majid bin Said na kujenga bandari na kisha kuupa mji jina hilo jipya miaka ya 1860.
Lipo pia eneo la Mwananyamala linalotokana na lugha ya Kizaramo likimaanisha mwana nyamaza.
Maeneo yaliyochukua majina ya watu
Aidha, yapo maeneo pia yaliyochukua majina ya watu. Msasani kwa mfano, asili yake ni mtu aliyeitwa Mussa Hassan, sawa na Shekilango ambalo ni kumbukumbu ya Hussein Ramadhan Shekilango, aliyewahi kuwa Mbunge wa Korogwe na waziri miaka ya 1970.