Nahodha: Mwinyi alileta matumaini kwenye nyakati ngumu

Waziri Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha

Muktasari:

Viongozi na maelfu ya wananchi wamejitokeza kuaga mwili wa Rais mstaafu wa awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi, hafla hiyo imefanyika katika uwanja wa New Amaan, Complex Zanzibar na anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake Mangapwani.


Unguja. Waziri Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha, amesema hayati Ali Hassan Mwinyi, alileta matumaini kwa wananchi katika nyakati ngumu walizokuwa wakipitia.

Nahodha amebainisha hayo leo Jumamosi Machi 2, 2024 katika hafla ya kumuaga kiongozi huyo inayofanyika katika uwanja wa New Amaan Complex  Zanzibar, ambapo viongozi na maelfu ya wananchi wamehudhuria kutoa heshima zao za mwisho.

Hayati Mwinyi alifariki Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na mazishi yanatarajiwa kufanyika leo Machi 2, 2024 nyumbani kwake, Mangapwani, Zanzibar.

Akizungumzia alivyomfahamu Mzee Mwinyi, Nahodha amesema alipoingia madarakani baada ya Rais Abdul Jumbe kujiuzulu mwaka 1984, alikuta hali mbaya ya uchumi na wananchi walikuwa na hali ngumu kimaisha.

Hata hivyo, amesema hayati Mwinyi aliweza kuleta matumaini kwa wananchi kwa kufungua uchumi kupitia mabadiliko aliyoyafanya na wananchi wakaanza kuona hali tofauti.

"Mungu alimpa baraka ya kufungua milango, pale palipofungwa akapafungua. Alikuwa mpole, msikivu na anayetoa matumaini. Kiongozi akiwa na mambo haya matatu, atapendwa na wananchi wake.

"Uongozi si kukurupuka, ni kutafakari na kufanya uamuzi. Mzee Mwinyi alikuwa na sifa hizo, tuendelee kumwombea apumzike kwa amani," amesema Nahodha wakati akizungumza na Mwananchi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka amesema wakati wa uongozi wake, alifanya kazi katika chama, hivyo alijifunza mchango wa kiongozi huyo katika kukijenga chama.

Amesema vijana wa sasa watapata historia kubwa ya Muungano wa vyama vya Tanu na ASP uliozaa CCM na namna alivyoiongiza serikali yake wakati wa hali ngumu ya uchumi.


"Wakati anaingia madarakani, IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa) walitofautiana na Mwalimu Nyerere, lakini alipoingia hayati Mwinyi, aliweka mambo sawa na hali ya maisha ya wananchi ikabadilika," amesema Ole Sendeka.

Ameongeza kwanza hakuwa na upendeleo, alifanya mambo kwa usawa. Amesema alikuwa mwanamageuzi aliyebadilisha hali ya maisha ya wananchi katika nafasi ya uongozi aliyokuwa nayo.

"Huyu mzee ni mwanamageuzi wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Sio ajabu kuona leo Rais wa Zanzibar ni mtoto wake, ni kwa sababu ya malezi yake aliyowapa," amesema Ole Sendeka.