Wananchi wamlilia Mzee Mwinyi, kumkumbuka kwa haya

Baadhi ya wananchi wakiwa wamejitokeza Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kuaga mwili wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

Muktasari:

  •  Mwili wa Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi (98) aliyefariki dunia jana Alhamisi utaagwa leo Ijumaa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kisha kusafirishwa kwenda Zanzibar kwa mazishi yatakayofanyika kesho Jumamosi

Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi waliofika kuaga mwili wa Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wamesema watamkumbuka kiongozi huyo kama mwasisi wa demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania.

Hatua kwa hatua mwili wa Mwinyi ukiagwa Uwanja wa Uhuru

Mzee Mwinyi alifariki dunia jana Alhamisi Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza siku saba za maombolezo kuanzia leo Ijumaa, Machi 1, 2024 ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti.

Pia, atazikwa kesho Jumamosi Machi 2, 2024 nyumbani kwake huko Mangapwani, Zanzibar baada ya wananchi na viongozi kupata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.

Hapa Dar es Salaam, shughuli ya kutoa heshima za mwisho inafanyika katika uwanja wa Uhuru huku wananchi na viongozi mbalimbali wa kitaifa watapata fursa ya kumuaga kiongozi huyo.

Wakimzungumzia kiongozi huyo, baadhi ya wananchi waliojitokeza kuaga wamesema Mzee Mwinyi alikuwa kiongozi mpole na mtulivu na atakumbukwa kwa kuasisi mageuzi katika Taifa hili.

Mkazi wa Mbagala, Yohana Chambili amesema amemfahamu Mzee Mwinyi kupitia simulizi alizosoma na kuambiwa na baba yake, hivyo alipokuwa mtu mzima ametambua kwamba ameacha alama kubwa hapa Tanzania.

"Mimi nimezaliwa wakati wa utawala wake, kwa hiyo, sikuwa nimekomaa kiakili wakati ule, lakini sasa nimesimuliwa na kusoma historia, sasa najua amefanya mengi ikiwemo kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

"Mimi na vijana wenzangu wengine tunaopiga siasa, huyu mzee ndiyo aliweka misingi hiyo. Tuendelee kumuenzi kwa kutambua kazi kubwa aliyoifanya wakati wa utawala wake," amesema.

Mkazi wa Temeke, Salum Mrisho amesema kupitia falsafa yake ya Ruksa", Mzee Mwinyi alifungua milango kwa kuruhusu bidhaa nyingi kuingia nchini ili kumaliza changamoto zote zilizokuwepo wakati huo.

"Nakumbuka tulikuwa tunaishi kama kisiwani, lakini akatubadilisha, tukaanza kuchangamana na wengine. Tukaanza kuona TV zinaanzishwa, mahitaji muhimu yakaanza kupatikana, vitu vingi ambavyo hatukuvijua tukaanza kuviona," amesema.


Ameongeza Mzee Mwinyi ndiye aliyeleta mageuzi ya kisiasa kwa kuanzisha mfumo wa vyama vingi na kwa mara ya kwanza Taifa likashuhudia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 wakati akimaliza muda wake.

Naye Tabitha Makasi amesema kiongozi huyo alikuwa mpole, msikivu na mwenye hotuba zinazofundisha na kuhamasisha watu kuwa na utu siku zote.

"Mwinyi alikuwa hana blahblah kama viongozi wengine, napenda ile hotuba yake ya maisha ya binadamu ni hadithi, alitukumbusha kitu muhimu sana katika maisha yetu. Apumzike kwa amani," amesema Tabitha.