Naibu Waziri akwama kwenye tope ubovu wa barabara, ashindwa kuhudhuria mkutano

Muktasari:
- Barabara hiyo ya kiwango cha changarawe, yenye urefu wa kilometa zaidi ya 40 kutoka Kwala mjini na ilipoharibika barabara hiyo ni kilometa tatu kabla ya kufika kijijini hapo.
Pwani. Msafara wa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Marryprisca Mahundi umekwama katika Kijiji cha Kimala Misale, Kata ya Dutumi, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani kutokana na ubovu wa barabara.
Msafara huo umekwama leo Ijumaa Mei 23, 2025 ambapo Waziri huyo alikuwa anakwenda kukagua hali ya upatikanaji wa mawasiliano katika kijiji hicho na kuzungumza na wananchi.
Barabara hiyo ya kiwango cha changarawe, yenye urefu wa kilometa zaidi ya 40 kutoka Kwala mjini na ilipoharibika barabara hiyo ni kilometa tatu kabla ya kufika kijijini hapo.

Gari ya Polisi iliyokuwa kwenye msafara wa Naibu Waziri wa Mawasiliano na teknolojia ya Habari, Marryprisca Mahundi ikiwa inanasuliwa baada ya kukwama kwenye tope katika kijiji cha Kimala Misale Kata ya Dutumi wilaya ya Kibaha Vijijini, mkoani Pwani kutokana na ubovu wa barabara.
Mwananchi limeshuhudia magari yakipata shida kupita katika baadhi ya maeneo na yalishindwa kuendelea na safari kutokana na barabara kujaa matope huku mengine yakinasa, likiwemo gari la Jeshi la Polisi.
Akizungumzia hali hiyo, mkazi wa kijiji hicho, Zaina Mbegu amesema barabara hiyo inawaathiri hasa wanawake wanapokwenda kujifungua.
Kutokana na hilo, amesema baadhi wamekuwa wakijifungulia barabarani au kufika hospitali kwa tabu.
“Tunaomba Serikali itusaidie suala la barabara kwa kuwa Kimala Misale ya sasa imekuwa kubwa ina huduma karibu zote za kijamii ikwemo maji, umeme na sasa mawasiliano lakini barabara imekuwa changamoto kubwa kwetu,” amesema Zaina.
Naye Adam Stephano ambaye ni mkulima, amesema ubovu huo wa barabara unasababisha kushindwa kusafirisha mazao ambayo soko lake kubwa wanategemea Mkoa wa Dar es Salaam.

Msafara wa Naibu Waziri wa Mawasiliano na teknolojia ya Habari, Marryprisca Mahundi ukiwa umesimama baada ya kushindwa kuendelea na safari kutokana ubovu wa barabara.
“Mwaka huu imebidi niuze mazao yangu kwa bei ya hasara, kwani mahindi badala ya kuuza debe Sh25,000 nauzia huku Sh15,000 wakati matikiti maji ndio kabisa yanaoza na nimepoteza zaidi ya Sh3 milioni nikizowekeza kwenye kilimo, kisa barabara,” amesema Adam.
Mbunge wa Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo amesema licha ya Waziri kukwama, mwenyewe atafika walipokuwa wananchi wakimsubiri na kufikisha salamu zake kwa kuwa kilometa mbili zilizobaki hata kwa mguu anafika.
Wakati kuhusu kujengewa mnara, amesema wanashukuru kwa kukumbukwa kwa niaba ya wananchi, huku akieleza wataalamu tayari walifika eneo hilo kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Alichosema Waziri
Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri Mahundi amelazimika kufanya mkutano na waandishi wa habari katika eneo hilo alipokwamia na kueleza nia ya ziara yake hiyo.
Waziri huyo katika mazungumzo yake hayo amesema alikuwa na shauku ya kwenda kuuzindua mnara huu ambao unajengwa na kampuni ya Yas (zamani tigo), baada ya kilio cha muda mrefu cha mtandao kutopatikana katika eneo hilo.
“Kama mnavyoona, nimefunga safari kuja huku licha ya changamoto za miundombinu ya barabara katika kufika lakini ndio hivyo, hapa tulipofika imeonekana safari haiwezi kuendelea tena,” amesema naibu waziri huyo.

Mbunge wa Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo, akizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Kimala Misale Kata ya Dutumi wilaya ya Kibaha Vijijini, mkoani Pwani
Pamoja na hayo amewapa Yas miezi mitatu kuanzia sasa kuhakikisha mnara huo unakamilika ili wananchi wapate mawasiliano ya uhakika.
Akizungumzia hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon amesema wanatambua ubovu wa barabara hiyo na tayari bajeti yake imetengwa kwa ajili ya kuitengeneza kwa kiwango cha lami.
“Ni kweli barabara hii tunaijua ni mbovu, ila tayari imeshatengewa bajeti yake ya kuitengeneza kwa kiwango cha lami, tulichokuwa tunasubiri ni hizi mvua zikatike,”amesema Simon.
Kuhusu ujenzi wa mnara, amesema hautasaidia tu wananchi kupata mawasiliano, bali na kufanya shughuli zingine za kidigitali ikiwemo uandikishaji daftari la mpigakura, kulipa bili za maji na umeme na mambo mengineyo.
Meneja wa Mfuko wa Mawasiliano Kanda ya Pwani, Baraka Elieza amesema kukamilika kwa mnara huo, kijiji hicho kitakuwa kikipata mtandao wa 3G hadi 4G huku akiwapa pole kwa kuvumilia kukosekana kwa mawasiliano eneo hilo.
Mwakilishi wa Kampuni ya Yas, Simplicius Komba amesema Serikali imetoa zaidi ya asilimia 50 ya ujenzi wa mnara huo, na wanaahidi kumaliza ndani ya muda.
Wiki ijayo, amesema wataanza kupeleka malighafi kwa ajili ya ujenzi huo huku akieleza changamoto za barabara haziwezi kuwa sababu ya kuwakwamisha kwani tayari wamejenga minara zaidi ya 50 katika kipindi hiki cha mvua.