Naibu Waziri Mkuu aipa tano Sweden

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza kwenye hafla ya kuwasilisha ripoti ya mpango wa matumizi ya bayogesi na kuendeleza ushirikano kati ya ubalozi wa Sweden na Tanzania Jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Katika kuadhimisha miaka 60 ya ushirikano kati ya Serikali ya Tanzania na Sweden, Nchi hizo zimeahidi kuendeleza uhusiano, ushirikano na kuimarisha ukuaji katika sekta za kiuchumi, elimu, Afya na nishati nchini.

Dodoma. Katika kile kinachooneka ni uhusiano mzuri wa kidiplomasia baina ya Sweden na Tanzania, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko amepongeza nchi hiyo kwa kutoa jumla ya Sh194 bilioni katika mradi umeme vijijini ambapo 101,000 wamenufaika.

Dk Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2023 wakati akizindua ripoti ya utafiti wa ushirikiano kwenye sekta ya nishati kati ya Tanzania na Sweden kwa miaka 60, huku akiisifu nchi hiyo kwa mchango wake katika kuisaidia Tanzania katika miradi mbalimbali.

"Sweden imekuwa ni moja ya nchini muhimu inayochangia kwa kiasi kikubwa kwenye miradi ya Nishati hususani umeme na imechangia Sh142 bilioni kwenye miradi ya ujazilizi kwenye vitongoji 1328 na katika vijiji takriban 151, imechangia Sh52 bilioni," amesema Dk Biteko.

Aidha, kuhusu uwekezaji Dk Biteko amesema kuwa katika sekta ya nishati, kwa sasa wanajipanga kuongeza nguvu ya uwekezaji huku akiwataka wadau katika sekta hiyo kuitumia vizuri fursa ya mikopo na misaada ya wadau wa maendeleo kama Sweden ili kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wa Balozi wa Sweden nchini, Charlotta Ozaki amesema uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden uliasisiwa na Waziri Mkuu wa Sweden kwa wakati huo, pamoja na Mwalimu Julius Nyerere ambaye ni Rais wa awamu ya kwanza wa Tanzania, ambapo walisaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano, unaoendelea mpaka leo.

Balozi Charlotta amesema kuwa tangu ushirikiano huo uanze mwaka1963 hadi leo 2023, nchi hiyo imetoa misaada yenye thamani ya takriban dola bilioni nane, ambazo zimetumika katika kusaidia sekta ya nishati ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya umeme na miradi ya umeme vijijini.